Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kituo cha kikanda cha kukabili Ebola chapatiwa dola 500,000

UNICEF inasema watoto wameathirika mno na mlipuko wa Ebola mashariki mwa DRC.
WHO/Lindsay Mackenzie
UNICEF inasema watoto wameathirika mno na mlipuko wa Ebola mashariki mwa DRC.

Kituo cha kikanda cha kukabili Ebola chapatiwa dola 500,000

Afya

Fuko kuu la misada ya dharura ya Umoja wa Mataifa, CERF hii leo limetoa dola 500,000 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa kituo cha pamoja cha kukabili na kuchukua hatua dhidi ya Ebola katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kituo hicho kitajengwa kwenye mji wa Entebbe nchini Uganda, ambapo mratibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Mark Lowcock amesema kituo hicho kitaongozwa na shirika la mpango wa chakula duniani, WFP kwa niaba ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia.

Bwana Lowcock amesema, “kituo hicho kitasaidia mataifa yaliyo jirani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambayo ni kitovu cha mlipu wa Ebola na jukumu kuu ni kusaidia kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo hatari iwapo kitahitajika kufanya hivyo. Kituo pia kitasaidia harakati za kudhibit mlipuko wa Ebola  huko DRC.”

Mkurugenzi wa WFP kanda ya Afrika Mashariki Erika Joergensen amenukuliwa kwenye taarifa iliyotolewa leo na WFP mjini Nairobi, Kenya akisema kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka na “nasihi wahisani wasaidia maandalizi na hatua za dharura dhidi ya Ebola ili tuutokomeze.”

Mchango huo wa CERF ni sehemu ya dola milioni 10.5 zinazotakiwa ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea kutokana na mlipuko wa sasa aw Ebola iwapo utaenea zaidi ya DRC.

Katika fedha hizo, dola milioni 3.8 zimepatiwa Uganda, dola milioni 2.4 Burundi, dola milioni 2 Sudan Kusini, dola milioni 1.8 Rwanda, kando mwa dola 500,000 za kituo hicho.

Fedha hizi zitasaidia hatua za haraka na kuchagiza mikakati ya maandalizi, ufuatiliaji, uhamasishaji umma, mawasiliano kuhusu hali halisi, kampeni za chanjo na mafunzo kwa wahudumu wa afya.

Mlipuko wa sasa wa Ebola huko DRC uliotangazwa Agosti Mosi mwaka 2018, ni wa pili kwa ukubwa zaidi kwenye historia ya Ebola nchini humo ambapo hadi sasa kati ya wagonjwa takribani 900 walioripotiwa, zaidi ya 560 wamefariki dunia.