Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Japo pengo la usawa linaweza kusambaratisha mihilili ya UN, haki inaleta matumaini:Bachelet

Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa akihutubia Machi 6, 2019 Kikao cha Baraza la Haki kuhusu hali ya haki za binadamu duniani.
UN /Violaine Martin
Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa akihutubia Machi 6, 2019 Kikao cha Baraza la Haki kuhusu hali ya haki za binadamu duniani.

Japo pengo la usawa linaweza kusambaratisha mihilili ya UN, haki inaleta matumaini:Bachelet

Haki za binadamu

Ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaendelea kutamalaki katika sehemu mbalimbali duniani ukichochewa zaidi na changamoto zilizopo hivi sasa ikiwemo tishio la mabadiliko ya tabianchi, maendeleo ya teknolojia, vita vinavyozua zahma kubwa kwa raia, ukosefu wa ajira kwa vijana, mabadiliko ya mifumo, chuki dhidi ya wageni na ongezeko la pengo la usawa.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka ya hali ya haki za binadamu duniani iliyowasilishwa leo mjini Geneva Uswisi na Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet.

Mbele ya nchi wanachama kwenye Baraza la Haki za binadamu Bi. Bachelet amesema changamoto kubwa zaidi hii leo ni ongezeko la pengo la usawa kwani“pengo la usawa katika kipato, mali, rasilimali, fursa ya haki ya kisheria vinaleta changamoto kubwa katika misingi ya usawa, utu na haki za binadamu kwa kila mtu, na vinatokana na uongozi mbovu, ufisadi, kutokuwepo utawala wa sheria, ubaguzi, na taasisi dhoofu au zenye upendeleo.”

Upatikanaji wa chakula nao ni mgumu mjini aza kutokana na umaskini, usalama mdogo na ukosefu wa ajira.
WFP/Wissam Nassar
Upatikanaji wa chakula nao ni mgumu mjini aza kutokana na umaskini, usalama mdogo na ukosefu wa ajira.

Athari za pengo la usawa katika jamii

Pia amesema pengo hilo katika masuala ya haki za kisiasa, kijamii na kiuchumi ni chachu na linaweza kusambaratisha mihimili ya Umoja wa Mataifa . Na ili kuhakikisha hili halitokei Bi. Bachelet amesema ni muhimu sana kufanyakazi kwa karibu na nchi wanachama na kuzisaidia kuweka mifumo ya usawa na kuhakikisha haki za binadamu zinadumishwa na kusisitiza kwamba,“pengo la usawa linaathiri nchi zote hata kattyika nchi tajiri watu bado wanahisi wanatengwa katika faida za maendeleo na kunyimwa haki za kiuchumi na kijamii na kusababisha hali ya kutengwa, na wakati mwingine machafuko.”

Pia ameongeza kuwa pengo hilo la usawa ni tishio kubwa la amani na usalama na limewalazimisha mamilioni ya watu kufungasha virago kuzihama nyumba zao na hata nchi zao. Amesisitiza kuwa pengo hilo la usawa limedumaza maendeleo ya kijamii, utulivu wa kiasiasa na kiuchumi.

Kwa upande mwingine akisema kudumisha amani kunajenga matumaini, kunawaleta watu pamoja katika misingi ya kuwa na mustakabali bora tofauti kabisa na ukandamizaji, ubaguzi, uonevu na kutokuwepo kwa usawa.

Kinachoendelea mashinani

Katika ripoti yake Kamishina Mkuu wa haki za binadamu akazigeukia nchi ambazo zimekuwa na changamoto kubwa ya masuala ya haki za binadamu ikiwemo suala la usawa mfano, “Nchini Sudan katika miezi kadhaa iliyopita watu ambao wamekuwa wakiandamana kupinga hali mbaya ya uchumi na utawala mbovu , wametawanywa kwa nguvu na vikosi vya usalama, wakati mwingine kwa kutumia risasi za moto. Matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati mwingine ndani ya hospitali , misikinini na kwenye vyuo vikuu , watu kuswekwa rumande kiholela, utesaji na kutangazwa kwa hali ya dharura, hakutasaidia kumaliza madukuduku halisi ambayo waandamanaji wanataka kuyaeleza. »

Kwa mantiki hiyo Umoja wa Mataifa unaichagiza  Sudan kufanya mabadiliko yyenye manufaa  kukabiliana na ufisadi uliotawala nchini humo, kufungua fursa za kiraia , kuwezesha majadiliano jumuishi na ushiriki mkubwa wa watu katika ngazi ya maamuzi.

Nchini Zimbabwe ambako changamoto za haki za binadamu zimekuwa kwa miaka nenda rundi ameweka bayana kwamba, « Maandamano ya kupinga hatua za kukabiliana na mdororo wa uchumi yalikabiliwa ghasia zisizokubalika kutoka kwa vikosi vya usalama lakini hatua za serikali za kuzindua mchakato wa majadiliano  katika siku za hivi karibuni zinatia moyo lakini nahofia ripoti za msako wa nyumba kwa nyumba pamoja na vitisho dhidi ya wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu na wanaowawakilisha watu waliokamatwa. »

Wakimbizi na wahamiaji wa Venezuela wakivuka daraja la Simon Bolivar nchini Veneuela.
UNHCR/Siegfried Modola
Wakimbizi na wahamiaji wa Venezuela wakivuka daraja la Simon Bolivar nchini Veneuela.

Mada zingine zilizoainishwa na ripoti

Ripoti hiyo ya kina, mbali ya kujikita na pengo la usawa imeangazia mada zingine ikiwemo hali mbaya ya kiuchumi, na haki za kisiasa na kiraia nchini Venezuela, Nicaragua, huku ikisikitishwa na wanayotendewa watetezi wa haki za binadamu kote duniani hususan Saudi Arabia na Uturuki.

Haki ya maendeleo na ajenda ya 2030 ya kutomwacha yeyote nyuma pia imegusiwa jicho likielekezwa kwa Uchina kuhakikisha safari hiyo inamjumuisha kila mmoja na hata jamii za walio wachache mfano nchini India. Mada za ugaidi, ukatili wa kingono kwenye migogoro na ongezeko la wimbi la wahamiaji hususan Amerika ya Kati, Marekani, Australia na Muungano wa Ulaya halikupewa kisogo.

Kwa mujibu wa ripoti suala la ugaidi lbado ni mtihani mkubwa dunia nziama ikiwemo katika nchi za Kiarabu, sahel na pembe ya Afrika. Lakini imehitimishwa kwa habari Njema zinazotia matumaiani hasa katika ukombozi wa mwanamke kwa nchi kama Ethiopia iliyopiga hatua, Tunisia ambayo karibuni imechagua Meya mwanammke na ongezeko la wabunge wanawake kwenye Bunge la Congress nchini Marekani.