Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yasaidia zaidi ya watu 130,000 walioathiriwa na mabadiliko ya tabianchi Burundi

Helikopta ya WFP ikisambaza chakula
UNICEF/Peter Martell
Helikopta ya WFP ikisambaza chakula

WFP yasaidia zaidi ya watu 130,000 walioathiriwa na mabadiliko ya tabianchi Burundi

Tabianchi na mazingira

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP linasambaza msaada wa dharura wa chakula kwa watu 134,000 waliokumbwa na uhaba wa chakula kutokana na mabadiliko ya tabianchi huko jimbo ni Kirundi nchini Burundi.

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo mjini Bujumbura, Burundi imesema shirika hilo kwa ushirikiano na shirika la maendeleo ya kimataifa la Marekani, USAID walianza kusambaza msaada huo kwa familia zinazokumbwa na uhaba wa chakula kwenye maeneo ya Busoni, Bugabira na Kirundo ili kuhakikisha wana mlo wenye lishe angalau kwa mwezi mmoja.

Mwakilishi wa WFP nchini Burundi Virginia Villar Arriban akinukuliwa kwenye  taarifa hiyo amesema  “kiwango cha madhara ya ukame huko Kirundo kinatisha. Tunachukua hatua kusaidia familia na kuzuia madhara haya yasiathiri zaidi familia zilizo hatarini.”

Katika tathmini yao huko Kirundo, WFP na Gavana wa jimbo hilo pamoja na wawakilishi kutoka wizara ya kilimo ya Burundi walibaini kuwa idadi kubwa ya kaya maeneo matatu ya jimbo hilo walipoteza mavuno yao kutokana na uhaba wa mvua wakati wa msimu wa upanzi mwaka uliopita wa 2018.

“Familia hazina mbinu za kupata chakula na pia hazina fursa za kufanya kazi. Masoko yako matupu na bidhaa chache zilizopo zinauzwa kwa bei ya juu sana. Matokeo yakeo, familia haziwezi hata kupata mlo mmoja kwa siku. Baadhi wameondoka Kirundo ili kusaka bidhaa au ajira kwenye majimbo ya jirani,” imesema taarifa hiyo.

WFP inasema hali inaweza kuwa mbaya zaidi wakati wa msimu wa mwambo kuanzia mwezi ujao wa Aprili hadi Mei kwasababu wakulima wamepoteza mavuno yao na hawana mbegu za kutumia wakati wa msimu ujao wa upanzi.

 “Kwa kwlei mimi mwenyewe nilistaajabu na hali niliyoiona lakini niliguswa sana na jinsi wanawake walivyo mstari wa mbele kufanya kila juhudi kusaidia familia zao licha ya hali ngumu wanayokabiliana nayo,” amesema Villar Arribas akiongeza kuwa familia nyingi zimesema zililazimika kuuza mali zao ikiwemo mifugo, ardhi na nyuma na sasa hawana pa kuishi na wamesalia maskini.

Tathmini iliyofanyika imeanisha kuwa misaada isambazwe kwamba kwa familia. Hata hivyo watoto wenye utapiamlo walio na umri wa chini ya miaka mitano pamoja na wanawake wajawazito na wale wanaonyonyesha watapatiwa chakula cha ziada.

Halikadhalika maji ya kunywa na misaada ya zana za kilimo pia itasambazwa bila kusahau kuimarisha mifumo ya afya.

Hata hivyo WFP imesema ili iweze kuendelea na usaidizi huo kwa miezi minne zaidi kuanzia mwezi Aprili, inahitaji dola milioni 7.