Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa IFAD kukomboa wakulima na mazao yao Rwanda

Kilimo bora Afrika ni mojawapo ya nchi za kunufaisha wakulima katika soko la pamoja.
FAO/Olivier Asselin
Kilimo bora Afrika ni mojawapo ya nchi za kunufaisha wakulima katika soko la pamoja.

Mradi wa IFAD kukomboa wakulima na mazao yao Rwanda

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Rwanda wakulima wanapoteza hadi asilimia 30 ya mazao yao kabla hata ya kufika sokoni kwa sababu ya ukosefu wa mbinu za kisasa za kukausha, kuhifadhi na kusafirisha mazao. Hali hiyo imesababisha mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD kusaidia wakulima kukabiliana na changmoto hiyo kwa kukarabati maghala na vituo vya kupokea mazao. Grace Kaneiya na maelezo zaidi.

Ni shughuli za kila siku shambani ambapo, viazi vilivyooza, mahindi na maharagwe, matokeo ya moja kwa moja ya ukosefu wa mbinu za uhifadhi isitoshe mabadiliko ya tabianchi na mvua kubwa yanasababisha hali kuwa mbaya zaidi. Mukamusana Siphora ni mkulima wa viazi na anasema, “wakati viazi vyetu vikinyeshewa na kupata maji vinaanza kuoza halafu sehemu ambayo ninaweza kuviuza haraka iwezekanavyo ni katika soko jirani.”

Kwa wakulima wa mahindi hali ni kama hiyo kwani uhifadhi waliokuwa wakifanya awali unakwamishwa na mvua kubwa. Gashema Venuste ni mkulima wa mahindi ambaye anafafanua kuwa, “Wakati mwingine mahema ambayo tulikuwa tunatumia kufunika mazao yanasombwa na mvua kubwa hadi mvua inaharibu mazao na mahindi yanaanza kuota. Hii hutokea wakati yanakaushwa. Katika kila kilo 100 tunapoteza takriban kilo 20.”

Ni katika kurekebisha hilo ambapo IFAD kwa ushirikiano na serikali ya Rwanda wamefadhili biashara ndogondogo 200 na vyama vya ushirika katika kuimarisha mijengo ikiwemo kukarabati maghala ya kukausha mahindi na kuhifadhi viazi na mafunzo kwa wakulima 16,000 kuhusu namna ya kuhifadhi mazao baada ya mavuno. Zeinab Uwizeyimana ni rais wa moja ya vyama vya ushirika.

“Inafurahisha kwamba kituo hiki kipya cha kukausha mazao kitatusaidia kukausha mazao yetu vizuri ili wanunuzi waje watusake sisi, sio sisi kuwafuata wao kwa sababu mazo yetu hayatakuwa na kuvu”.

Mradi huu unatarajiwa kulenga wakulima 32,000 nchini humo.