Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi siku hizi hazipinduliwi na majeshi, ni takwimu-Dkt Albina Chuwa

Mkurugenzi Mkuu wa ofisi ya Takwimu Tanzania, Albina Chuwa wakati wa mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kando ya mkutano wa 50 wa Kamisheni ya Takwimu ya UN jijini New York, Marekani.
UN/Patrick Newman
Mkurugenzi Mkuu wa ofisi ya Takwimu Tanzania, Albina Chuwa wakati wa mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kando ya mkutano wa 50 wa Kamisheni ya Takwimu ya UN jijini New York, Marekani.

Nchi siku hizi hazipinduliwi na majeshi, ni takwimu-Dkt Albina Chuwa

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa kila mwaka wa wakuu wa ofisi za takwimu za nchi kote duniani unaendelea katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa hapa mjini New York Marekani. Mkutano huu hutumika kujadili namna takwimu zinavyoweza kuchangia katika maendeleo ya watu kote duniani.

Miongoni mwa wanaohudhuria mkutano huu ni Mkurugenzi Mkuu wa ofisi ya Takwimu nchini Tanzania, NBS, Dkt Albina Chuwa ambaye akihojiwa na UN News alianza kwa kueleza umuhimu wa takwimu katika maisha ya kila siku, "katika ngazi ya kaya yaani mtu binafsi kama ninapika chakula nyumbani siwezi mchele kilo 20 nikauweka kwenye sufuria nikapika wakati nina watu watatu pale ndani, kwa hivyo utakuta takwimu ni maisha yako ya kila siku. Huwezi kufanya maisha yako yoyote yale bila kutumia takwimu, huwezi na ndiyo kitu tunachokijadili hapa."

Kuhusu utofauti ya mkutano wa sasa ambao ni wa 50 tangu utaratibu wa wakuu wa ofisi za nchi zinazohusika na takwimu kukutana katika Umoja wa Mataifa, Dkt Albina Chuwa anasema, "mkutano wa mwaka huu unalenga sana katika utekelezaji wa malengo endelevu ya dunia, SDGs, kwasababu sasa hivi kuna mapitio ya kuona nchi zimefikia wapi katika utekelezaji wa malengo hayo.  Kwa mfano nchi yetu ya Tanzania tuna ripoti mwaka huu mwezi Juni. Na kitu kizuri ni uhusiano wetu tuliokuwa nao na haya mashirika kama UNDP, UNFPA ambao kwa Tanzania tunafanya nao kazi kwa pamoja kuhakikisha kwamba taarifa yetu inakaa sawa kwa ajili ya kuja kuiwasilisha hapa New York mwezi wa Juni mwaka huu 2019."

Na je kwa uzoefu wake wa miaka 30 katika tasnia hii anaona ni kwa namna gani yanayojadiliwa kaatika mkutano huu yataweza kusaidi kufanikisha SDGs, Dkt Albina Chuwa anafafanua, " Mimi kwanza nimefurahi, hii mnayoiita Ukumbi wa General Assembly mimi ni mara yangu ya kwanza kuingia humu,  awali tulikuwa tunawekwa huko chini lakini hivi tumekuja kukutana humu, manake nini? Manake ni  kuwa sasa takwimu imepata utashi wa kisiasa. Nchini Tanzania ninaona rais anavyotilia mkazo katika takwimu rasmi za nchi. Nchi yoyote haipinduliwi tena na majeshi, ni takwimu tu. Ukitoa takwimu za ajabu watu wataandamana tu. Kwa hivyo utashi wa siasa ulioanzia katika Umoja wa Mataifa unashuka hadi chini. Hata katika Afrika Mawaziri wa fedha na mipango ya Afrika waliazimia kuwa takwimu ikae juu na ndiyo muongozo. Ninapomsikia rais wangu anatoa hotuba yake anatumia takwimu nakushukuru Mungu nasema sasa takwimu imeingia. Siyo kama zamani watu walikuwa wanapanga kwa kutumia uzoefu. Huwezi!"