Mahitaji ya kibinadamu yameongezeka Burkina Faso, hatua zaidi zahitajika- Mueller

5 Machi 2019

Naibu Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu, OCHA Ursula Mueller yuko ziarani nchini Burkina Faso ambakoamesema mahitaji ya kibinadamu yameongezeka kwa kiwango cha juu tangu mwezi Juni mwaka jana 2018 na katika miezi ya hivi karibuni.

 

Bi. Mueller amenukuliwa na msemaji wa OCHA mjini Geneva, Uswisi, Jens Laerke, akisema kuwa hali hiyo ni kufuatia ongezeko la ukosefu wa usalama ikichochewa na uwepo wa vikundi vilivyojihami na mizozo baina ya jamii mbalimbali katika maeneo ya kaskazini ya kati na mashariki mwa Burkina Faso .

Kwa mujibu wa OCHA, Burkina Faso inakabiliwa na mzozo wa wakimbizi wa ndani huku zaidi ya watu 100,000 wamefurushwa makwao na zaidi ya nusu wakikimbia katika kipindi cha miezi miwili iliyopita pekee.

Aidha zaidi ya watu 120,000 hawapati huduma za afya na wengine 670,000 wako katika hatari ya kukumbwa na njaa, watoto 130,000 wakikabiliwa na utapiamlo uliokithiri mwaka huu wakati shule zimefungwa na kuwanyima watoto 150,000 fursa ya kupata elimu.

OCHA imesema kufikia mwishoni mwa mwezi uliopita wa Februari, takriban watu 1.2 walikuwa wanahitaji msaada nchini Burkina Faso.

Mamlaka nchini Burkina Faso na watoa misaada wametoa msaada, lakini hatua zaidi zahitajika kufanyika kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watu walioathirika, amesema Bi. Mueller.

Mwezi uliopita,  serikali na watoa msaada walizindua ombi la dharura la dola milioni 100 kwa ajili ya kusaidia watu 900,000 wanaokabiliwa na mzozo ambapo hadi  kufikia sasa ombi hilo limefadhiliwa kwa asilimi 16 tu.

Jumatatu wiki hii mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF umetoa milioni 4 kwa ajili ya kuimarisha msaada kwa wakimbizi wa ndani, jamii zinazowahifadhi na utoaji wa huduma kwa wanawake na wasichana 15, 500.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter