Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado tuko mbali kufikia tiba ya UKIMWI lakini hatua ya sasa imetupa matumaini-UNAIDS.

Mtoto mchanga akitolewa sampuli za damu ili apimwe VVU katika moja ya vitu vya kuchunguza Virusi Vya Ukimwi, VVU huko Kyrgyzstan
UNICEF/Aleksei Osipov
Mtoto mchanga akitolewa sampuli za damu ili apimwe VVU katika moja ya vitu vya kuchunguza Virusi Vya Ukimwi, VVU huko Kyrgyzstan

Bado tuko mbali kufikia tiba ya UKIMWI lakini hatua ya sasa imetupa matumaini-UNAIDS.

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya UKIMWI, UNAIDS  limesema limetiwa moyo na ripoti iliyochapishwa leo mjini Seattle Marekani na Geneva Uswisi ya mgonjwa wa aliyekuwa na ukimwi kuponywa  

Kwa mujibu wa UNAIDS mwanaume huyo alikuwa akipewa tiba tangu mwaka 2016 na wataalamu katika Chuo Kikuu cha London na Chuo Kikuu cha Imperial kinachohusika na magonjwa ya saratani.

Mkurugenzi mkuu wa UNAIDS Michel Sidibé  amenukuliwa akisema “ kupata tiba ya Virusi vya UKIMWI ni ndoto ya mwisho. Ingawa hatua hii bado ni ngumu na kazi kubwa zaidi inahitajika, inatupa matumaini makubwa kwa siku za usoni tunaweza kuumaliza UKIMWI kwa njia za sayansi kupitia chanjo au tiba. Hata hivyo inatuonesha ni kiasi fgani bado tuko mbali kufikia hapo na pia umuhimu wa kuendelea lijikita katika juhudi za kuzuia VVU na kutibu.”

Taarifa ya UNAIDS ikifafanua kuhusu hatua ya sasa, imesema upandikizaji wa seli ni jambo gumu, tete la gharama na lenye athari zitokanazo na tiba hiyo kiasi cha kutokuwa njia inayoweza kuwatibu watu wengi walio na virusi vya UKIMWI. Hata hivyo inaelezwa kuwa matokeo ya sasa yanatoa mwelekeo mzuri kwa watafiti wanaoshughulika na VVU na pia kuonesha umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika utafiti wa kisayansi dhidi ya Virusi hivyo.

Assumpta Massoi/UNNewsKiswahili
Naishi na VVU bila woga hivi sasa

Matokeo haya yametangazwa katika kongamano lililofanyika mjini Seattle Marekani linalohusu virusi vyenye tabia ya kujibadilisha ndani ya mwili ili kijifananisha na hali halisi ya mwilini ili viweze kuzaliana na kushambulia viungo vya asili kama seli. Matokeo ya mgonjwa ya kwanza kabla ya haya ya sasa, yalikuwa ya Timothy Ray Brown ambaye alipokea matibabu ya saratani mwaka 2007.

Hata hivyo tarifa ya UNIDS imesisitiza kuwa ulimwengu ni lazima utambue kuwa hivi sasa bado hakuna tiba ya Virusi vya UKIMWI.

UNAIDS inafanya kazi kuhakikisha watu wote wanaoishi na walioathirika na VVU wanapata huduma za dawa za kurefusha maisha na matibabu. Takwimu zinaonesha mwaka 2017 kulikuwa na watu milioni 36.9 waliokuwa wakiishi na VVU na watu milioni 1.8 walipata maambukizi mapya huku katika mwaka huo huo takribani watu milioni 1 walikufa kutokana na magonjwa yaliyohusiana moja kwa moja na UKIMWI.