Elimu jumuishi ni zaidi ya kuwajumuisha watoto wenye ulemavu na wenzao- Bachelet

Anupriya akishiriki kwenye michezo katika kituo cha Anaganwadi nchini India. Kupitia mtaala ulioboreshwa, watoto wanashiriki kwenye michezo ya kuboresha uwezo wao wa kuelewa lugha na utambuzi.
UNICEF/UN0280961/Vishwanathan
Anupriya akishiriki kwenye michezo katika kituo cha Anaganwadi nchini India. Kupitia mtaala ulioboreshwa, watoto wanashiriki kwenye michezo ya kuboresha uwezo wao wa kuelewa lugha na utambuzi.

Elimu jumuishi ni zaidi ya kuwajumuisha watoto wenye ulemavu na wenzao- Bachelet

Haki za binadamu

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao mahsusi kuhusu haki za mtoto likiangazia jinsi ya kuwawezesha watoto wenye ulemavu kupitia elimu jumuishi.

Akihutubia kwenye mkutano huo wa 40 wa Baraza la Haki za Binadamu, Kamishan Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amesema mafanikio makubwa yamepatikana tangu kupitishwa kwa mkataba wa haki za mtoto, CRC mwaka 1989 ambapo mataifa yaliyoridhia yamepitisha sheria na kanuni za kulinda haki za mtoto.

Hata hivyo amesema miaka 30 tangu kupitishwa kwa CRC bado kuna ukweli mchungu ya kwamba “mamilioni ya Watoto wanaendelea kunyimwa haki zao kila uchao, na idadi kubwa ya Watoto hao ni wale wanaoishi na ulemavu.”

Amesema ni ukweli ulio wazi kuwa takribani Watoto milioni 93 wenye ulemavu wako kwenye hatari kubwa zaidi haki zao kukiukwa tangu tu wanapozaliwa

“Uzazi wao unaweza usisajiliwe. Wanaweza kuwekwa kwenye taasisi ambazo zinakiuka haki zao za kuwa na familia, au wasipatiwe elimu jumuishi na wako hatarini kukumbwa na ukatili na kupuuzwa,” amesema Bi. Bachelet.

Ameongeza kuwa sauti zao zinaweza zisisikilizwe hata kwenye hoja za msingi kuhusu pale wanapoishi, je wanaishi na nani na maslahi yao ni yapi akisema hali ni mbaya zaidi kwa watoto wenye ulemavu wanaoishi kwenye maeneo yenye mizozo na yale yenye majanga ya kibinadamu.

Hata hivyo Bi. Bachelet amesema katika mazingira  yenye changamoto kama hayo, jawabu ni moja pekee, “kuongeza maradufu ahadi yetu ya kuwezesha Watoto, wakiwemo wale wenye ulemavu ili waweze kufurahia haki zao za msingi.”

“Uwezeshaji ni pamoja na njia za kufanikisha na matunda ya kupata haki za binadamu. Inawezesha watoto kujumuishwa kwenye familia na jamii zao. Inahakikisha kuwa wanalindwa dhidi ya ghasia na ukatili. Zaidi ya yote inatoa hakikisho ya kwamba wanasikilizwa,” amesema Bi. Bachelet.

Amepigia chepuo elimu jumuishi akisema, “ni njia bora ya kuwa na jamii jumuishi. Lakini kuna vikwazo ambavyo vinapaswa kueleweka na kutambuliwa ili viweze kuondolewa.

Ametaja vikwazo hivyo kuwa ni pamoja na shule kutokuwa na miundombinu ya kutosha au kutokuwa na miundombinu kabisa ya kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu kujumuika na wenzao.

“Elimu jumuishi siyo tu kuwaweka Watoto wenye ulemavu kwenye shule za kawaida na kuacha wao wenyewe kuhaha kuweza kumudu. Elimu jumuishi ni kuweka mifumo ambayo inawezesha watoto hao kumudu, kuwa na mbinu za ufundishaji za kuwawezesha kujifunza na waweze kujifunza kwa ukamilifu kama wenzao,” amesema Kamishna Mkuu Bachelet.

Bi. Bachelet amesihi wajumbe washirikiane kwa kina kuwezesha watoto waishi maisha yenye utu, wajenge ndoto zao, na waweze kuzifikia kwa mustakabali wao wenye nuru.