Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hewa chafuzi ni muuaji wa kimyakimya wa watu milioni 7 kila mwaka-Mtaalamu wa UN

Kiwango cha uchafuzi wa hewa ni cha juu kiasi kwamba mtoto huyu amelazimika kuvaa barakoa wakati akisubiri basi kwenye kituo kimoja huko Ulaanbaatar nchini Mongolia
UNICEF/Mungunkhishig Batbaatar
Kiwango cha uchafuzi wa hewa ni cha juu kiasi kwamba mtoto huyu amelazimika kuvaa barakoa wakati akisubiri basi kwenye kituo kimoja huko Ulaanbaatar nchini Mongolia

Hewa chafuzi ni muuaji wa kimyakimya wa watu milioni 7 kila mwaka-Mtaalamu wa UN

Tabianchi na mazingira

Zaidi ya watu bilioni 6 duniani, theluthi moja yao wakiwa ni watoto, mara kwa mara wanavuta hewa chafuzi, hali ambayo inaweka maisha, afya na ustawi wao hatarini, ameeleza hii leo mjini Geneva Uswisi mtaalamu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu na mazingira. 

Taarifa iliyochapishwa katika tovuti ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifaifa (OHCHR) imemnukuu bwana David Boyd akisema kuwa uchafuzi wa hewa, ndani na nje ya makazi, ni muuaji wa kimyakimya ambaye wakati mwingine haonekani na ambaye anasababisha vifo vya mapema kwa watu milioni 7 kila mwaka wakiwemo watoto 600,000.

“Tatizo hili haliangaliwi kwa uzito unaostahili kwasababu vifo vyake haviko kama vile vinavyosababishwa na majanga mengine. Kila saa watu 800 wanakufa, wengi baada ya mateso ya muda mrefu kutokana na saratani, magonjwa ya kupumua au ya moyo ambayo yamesababishwa moja kwa moja na uchafuzi wa hewa.” David Boyd ameliambia Baraza la Haki za binadamu mjini Geneva.

Boyd amesema kuwa kushindwa kuwahakikishia watu hewa safi kunakiuka haki yao ya msingi ya kuishi katika mazingira bora, haki ambayo inatambulika kisheria na nchi 155 na inatakiwa kutambuliwa kidunia, “watu hawawezi kukwepa kuvuta uchafu wowote ulioko katika hewa ndani ya nyumba zao au katika jamii zao. Uchafuzi wa hewa uko kila mahali, kwa kiasi kikubwa ukisababishwa na kuunguza kwa mafuta ya mabaki ili kuzalisha nishati ya umeme, usafirishaji, kuzalisha joto, na pia kutoka katika shughuli za viwanda, udhibiti duni wa taka na shughuli za kilimo.”

Amesema wanawake na watoto katika nchi zenye kipato kidogo ambao muda mwingi wanakaa nyumbani, wanaathirika na uchafuzi wa hewa unaosababishwa na kupika, kuzalisha joto au mwanga kunakotokana na nishati ngumu au mafuta ya taa.

Aidha mtaalamu huyo amesisitiza kuwa uchafuzi wa hewa ni jambo linalozuilika na hivyo akatoa wito kwa nchi kutimiza ahadi zao za kuhakikisha hewa safi ambayo ni muhimu kutimiza hazi ya maisha, afya, maji na kujisafi, makazi bora na mazingira bora.

Bwana David Boyd ameeleza hatua saba ambazo nchi zinatakiwa kuchukua ili kuhakikisha kunakuwa na hewa safi na kuwahakikishia watu haki yao ya mazingira bora kuwa ni pamoja na kufuatilia ubora wa hewa na athari zake kwa afya ya binadamu, kuchunguza vyanzo vya uchafuzi wa hewa na kuweka wazi taarifa kwa jamii.

“Kuna mifano mingi mizuri kama vile programu nchini India na Indonesia ambazo ziliwasaidia mamilioni ya familia masikini kuhamia katika teknolojia bora za kupika na pia mataifa ambayo kwa mafanikio wamemaliza matumizi ya makaa yam awe. Hatua nyingi zaidi zinaweza kuchukuliwa ili kupunguza uchafuzi wa hewa ambao unasababisha mabadiliko ya tabianchi yanayoleta hasara mara mbili.” Amesisitiza bwana Boyd.