Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wanaendelea kubeba gharama ya vita Yemen licha ya usitishaji uhasama:UNICEF

Mama akiwa na watoto wake wakisubiri msaada wakati UNICEF ilipotoa msaada Hudaidah, Yemen, Juni 2018
UNICEF
Mama akiwa na watoto wake wakisubiri msaada wakati UNICEF ilipotoa msaada Hudaidah, Yemen, Juni 2018

Watoto wanaendelea kubeba gharama ya vita Yemen licha ya usitishaji uhasama:UNICEF

Amani na Usalama

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF, Henrietta Fore amesema vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen vinaendelea kuwabebesha watoto gharama kubwa ya maisha yao.

Fore ametoa kauli hiyo hii leo Jumamosi katika taarifa yake akilaani vikali shambulio lililokatili maisha ya watoto watano kwenye mji wa bandari wa Hudaidah siku ya Alhamisi wiki hii.


Katika taarifa hiyo Bi. Fore ameongeza kuwa “Watoto nchini Yemen hawana tena usalama wa kufanya vitu ambavyo kama Watoto wanastahili kufanya kama vile kwenda shuleni au kucheza na rafiki zao nje kwani vita vinawafikia kila waliko hata ndani ya nyumba zao,”


Pande kinzani katika mzozo wa Yemen zilitia saini makubaliano ya usitishaji uhasama kwa muda katika mwezi Disemba mwaka jana chini ya usuluhishi na usimamizi wa Umoja wa Mataifa , lakini mkataba huo haukuzuia kuuawa kwa watoto watano katika shambulio lililofanyika wilayani Tahita Kusini mwa mji wa Hudaidah, mji ambao ni muhimu sana kwa uingizaji wa misaada ambayo inahitajika kwa udi na uvumba ili kuokoa maisha ya mamilioni ya raia wa Yemen wasife na njaa.


Mkuu huyo wa UNICEF anasema “Kila siku watoto wanane wanauawa au kujeruhiwa katika maeneo 31 ambako vita vinaendelea nchini Yemen na mazungumzo na mikutano hadi sasa imesaidia kidogo sana kubadili hali halisi inayowakabili watoto nchini Yemen. Mkataba wa amani wa kina ndio njia pekee itakayowakinga na vita na ghasia watoto wa Yemen kitu ambacho wanakihitaji na kustahili.”

Mwanzoni mwa wiki Geert Cappelaere , mkurugenzi wa kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wa UNICEF alisema “Vita vinavyoendelea nchini Yemen havijamuhifadhi mtoto hata mmoja”.

Alitoa kauli hiyo siku moja tu kabla ya mkutano wa kimataifa wa ngazi ya juu wa kuchangisha fedha za usaidizi kwa ajili ya Yemen uliofanyika mjini Geneva Uswis na kufanikiwa kuchangisha dola bilioni 26 kusaidia janga la kibinadamu linaloendelea nchini humo.