Jeshi la wananchi Tanzania, JWTZ lanuia kutekeleza kwa vitendo lengo namba 4 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

1 Machi 2019

Umoja wa Mataifa kupitia lengo namba 4 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kuhusu elimu bora, unapigia chepuo elimu ambayo si tu jumuishi bali pia inampatia mnufaika stadi za kumkomboa kimaisha, iwe kwa kupata ajira akiwa ofisini au akiwa kwenye medani za nje. Nchini Tanzania, moja ya mataifa yaliyoridhia malengo hayo, jeshi la wananchi, JWTZ limeitikia wito huo kupitia shule ambazo inazimiliki. Luteni Kanali Semunyu wa JWTZ alishiriki kikao kilichosheheni maofisa wa ngazi mbalimbali za kijeshi pamoja na wale wanaoongoza taasisi za elimu zilizoko chini ya JWTZ.

Wakuu wa shule hizo wameweka maazimio nane yenye lengo la kuboresha shule ili kuzalisha wahitimu wanaoendana hali ya sasa inayohitaji ueledi wa hali ya juu katika nyanja mbalimbali hususani za viwanda.

Wakati wa kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es salam, Mkuu wa mafunzo na utendaji kivita Meja Jenerali Alfred Kapinga amewataka wakuu wa shule za kijeshi kuwa wabunifu kwa kuwaongezea wanafunzi  wao ujuzi wa fani zinazozunguka maeneo ya shule hizo kama masuala ya anga, majini, kilimo, magari na michezo.

Meja Jenerali Kapinga ameongeza kuwa shule za jeshi zina mazingira mazuri ya kujifunzia wakiwemo walimu wanajeshi hivyo lazima kuwe na utofauti  wa  namna ya utoaji wa elimu hasa suala la  nidhamu inayotokana na misingi ya  kijeshi.

Wakuu hao wa shule za Jeshi la Tanzania wameahidi kufanyia kazi maazimio hayo ikiwa  ni utekelezaji wa maagizo ya mkuu wa majeshi ya ulinzi Jenerali Venance Mabeyo ili kurejesha sifa na  majina ya shule za jeshi kwa kupata matokeo bora na kufuta daraja 0 na daraja la nne katika matokeo ya kidato cha nne na sita. 

Naye Meja Esau Lusulo mkuu wa shule Al Khamisi Camp iliyoko kisiwani Pemba.

Luteni Kanali Laurence Mgongolwa, mkuu wa shule Kigamboni naye alihudhuria kikao hicho.

Miongoni mwa maazimio yaliyowekwa ni uanzishaji wa masomo ya sayansi ya kijeshi, kusimamia ipasavyo walimu, nidhamu, uboreshaji miundombinu uanzishwaji wa klabu za hesabu, kufufua vipaji kwa shule za michezo na kuboresha uhusiano na wadau wengine wa elimu ili kuendana na mabadiliko. 

Shule zinazomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania ni Nyuki Unguja, Airwing, Makongo, Kigamboni  na Jitegemee iliyoko Dar eS salaam,   Kawawa ya Iringa, Unyanyembe Tabora, Ruhuwiko Songea, Al Khamis Camp Pemba  na Kizuka Morogoro 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter