Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Badilisheni sheria baguzi ili kurejesha utu na heshima ya binadamu- UNAIDS

Kijana anayeishi Peru aliyepatikana kuwa anaishi na VVU mapema mwaka 2018
© UNICEF/Daniele Volpe
Kijana anayeishi Peru aliyepatikana kuwa anaishi na VVU mapema mwaka 2018

Badilisheni sheria baguzi ili kurejesha utu na heshima ya binadamu- UNAIDS

Afya

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ubaguzi unaokwamisha mtu kupata  huduma za afya na nyinginezo, shirika la Umo wa Mataifa linalohusika na harakati dhidi ya Ukimwi, UNAIDS limetaka nchi zote duniani zichunguze sheria na sera baguzi zinazozuia baadhi ya makundi kupata  huduma hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Michel Sidibé amesema ukiukwaji wa haki unafanyika kote duniani kwa sababu ya uwepo wa sheria na matendo baguzi na kwamba sheria zinapaswa kulinda na si kuumiza.

Ametolea mfano kuwa mataifa 20 yameweka aina fulani ya vikwazo vya usafiri dhidi ya watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, VVU, mataifa mengine 29 yameripotiwa kuwa mwanamke anahitaji ridhaa ya mumewe au mpendwa wake ili aweze kupata huduma za afya ya uzazi.

Halikadhalika mataifa 59 yanalazimu makundi fulani ya watu kuchunguza hali yao ya VVU kabla ya ndoa, kuajiriwa au vibali vya kuishi na kama hiyo haitoshi kwenye mataifa yapatao 67, ndoa za  jinsia moja zimeharamishwa.

Ni kwa kuzingatia sheria na kanuni hizo kandamizi zilizopitishwa mwaka 2018 ambapo Bwana Sidibe anasema

“Nchi zote lazima zitathmini kwa kina sheria na será zao kuhakikisha usawa na ulinzi kwa watu wote bila ubaguzi wowote. Katika siku ya kutokomeza aina zote za ubaguzi na kila siku hebu na tuchukue hatua pamoja kubadili sheria baguzi.”

Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNAIDS amepongeza mataifa ambayo mwaka jana yalichukua hatua kubadili sheria baguzi akitolea mfano India ambako Mahakama Kuu ilifuta kifungu namba 377 cha Kanuni za makosa ya jinai ambacho kilikuwa kinaharamisha mahusiano  ya jinsia moja.

Nayo Ufilipino imeshusha umri wa ridhaa ya mtu kuchunguza VVU bila kusaka ridhaa ya mzazi au mlezi ambapo sasa ni umri wa miaka 15, ilihali nchini Malawi wameondoa kifungu cha sheria ambacho kingalimtia mtu hatiani iwapo asingalitangaza bayana kuwa ana VVU.