Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlo wa siku moja tu ni changamoto kwa wakimbizi na wasaka hifadhi Misri.

Wakimbizi mjini Cairo Misri
UNHCR/Scott Nelson
Wakimbizi mjini Cairo Misri

Mlo wa siku moja tu ni changamoto kwa wakimbizi na wasaka hifadhi Misri.

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika  la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR hii leo mjini Geneva Uswisi limesema msaada unaotolewa kwa wakimbizi walioko Misri uko katika wakati mgumu kutokana na kuongezeka kwa wakimbizi wapya huku kukiwa na vyanzo haba vya rasilimali.

UNHCR imefafanua kuwa migogoro inaoendelea nchini Yemen na katika nchi za Afrika zilizoko chini ya ukanda wa jangwa la Sahara, imewalazimisha watu wengi kukimbilia Misri.

Kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, idadi ya wakimbizi walioandikishwa na pia wale wanaosaka hifadhi nchini Misri imeongezeka kwa asilimia 24.

Taarifa ya UNCHR inasema hivi sasa programu za wakimbizi nchini Misri ambazo kimsingi zinalenga kuwasaidia na kuwalinda wakimbizi robo milioni, ambao zaidi ya nusu yao ni wasyria na wengine kutoka Sudan, Ethiopia, Eritrea, Sudan Kusini na Yemen.

Kamishina Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi amesema, “Ninaumizwa sana na ukweli kuwa wakimbizi 8 kati ya 10 nchini Misri wanaishi katika hali mbaya. Hawawezi hata kupata mahitaji ya msingi. Kupata tu chakula cha kila siku ni changamoto. Wakimbizi hawa wanahitaji msaada wa kibinadamu lakini hivi sasa hatuwezi kuwahudumia ipasavyo .”

 UNHCR imesema kwa miezi miwili katika mwaka huu wa 2019, imekuwa ikijiendesha kwa kiasi kidogo tu cha bajeti yake ya mwaka ya dola milioni 104.2.