Nchini Chad, madarasa ya wasichana pekee yasaidia kupunguza hofu na kuchagiza usawa wa jinsia

28 Februari 2019

Mwalimu amenyanyua mchoro wa msichana barubaru ambaye amegutuka tu na kubaini kuwa amechafua nguo yake kutokana na kupata hedhi ya kwanza akiwa shuleni. Mwalimu huyu anazungumza na wasichana walioko darasani kwenye mji wa Bol nchini Chad.

“Tumezungumza kuhusu kubalehe na hedhi na tukaangalia simulizi ya msichana ambaye kwa mara ya kwanza amepata hedhi,” Fatime Al Abakar amesema  hayo akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kwenye darasa lao la shule ya wasichana pekee ya Bol.

“Takribani wasichana 50 wako darasani. Wengi wao kama Fatime Ali Bakar tayari wameanza hedhi, lakini somo la leo lina umuhimu mkubwa,” amesema Houa Adoum Abdoulaye mwenye umri wa miaka 20. “Darasa hili linaweza kutuwezesha kusaidia wasichana ambao wanachanganyikiwa au wana hofu kuhusu kile ambacho kitawapata.”

Uhamasishaji

Somo hili  ambalo hufanyika baada ya saa za shule za kawaida limeandaliwa na kikundi cha waumini wanawake, kinachohusisha walimu waislamu ambao wana uhusiano wa karibu na Baraza la Juu la masuala ya kiislamu nchini Chad.

Lengo la kikundi hiki ni kuchangia katika kuelimisha kuhusu masuala yanayoathiri wanawake na wasichana, hususan  ukatili wa kijinsia, kuhamasisha kuhusu afya ya uzazi na hatari za misimamo mikali inayochagizwa na vikundi vyenye misimamo mikali kwenye ukanda wa Sahel.

Mariam Abakar ni Rais wa chama hicho kwa eneo la Lac ambako ndiko kunapatikana eneo la Bol lililo mstari wa mbele kwenye mafunzo kwa watoto wa kike. Ubadilishanaji wa taarifa unafanyika katika madrassa, ambalo ni darasa la kupatiwa wanafunzi elimu ya dini ya kiislamu.

Fatime Ali Abakar, mwenye umri wa miaka 22, amekuwa akijifunza kuhusu usawa wa kijinsia na madarasa hayo yanawezeshwa na shirika la idadi ya watu la Umoja wa Mataifa, UNFPA
UN /Eskinder Debebe
Fatime Ali Abakar, mwenye umri wa miaka 22, amekuwa akijifunza kuhusu usawa wa kijinsia na madarasa hayo yanawezeshwa na shirika la idadi ya watu la Umoja wa Mataifa, UNFPA

 “Katika ulimwengu wa kiislamu, wanawake wanatenganishwa na wanaume, hususan msikitini, kwa hiyo ni muhimu sana wanawake kukutana pamoja na kujadili masuala mengi ambayo yanatuathiri,” amesema Mariam.

Pindi darasa la masuala ya kubalehe linapokamilika, wasichana wanarejea  makwao ambako ukeketaji, ndoa za umri mdogo na ujauzito wa mapema vinakubalika kama tamaduni ambazo ni sehemu ya maisha yao nchini Chad.

Ndoa za umri mdogo

Takwimu kutoka Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa asilimia 30 ya wanawake wa Chad wenye  umri wa kati ya miaka 20-24 wanaozwa kabla ya kutimiza umri wa miaka 15. Katika kundi hilo hilo, asilimia 14 wanajifungua watoto kabla ya kutimiza umri wa miaka 15. Ukeketaji wa wanawake na watoto wa kike, ambao unatekelezwa katika sehemu kubwa ya Chad unaathiri asilimia 44 ya wanawake wote nchini humo.

Shirika la idadi ya watu la Umoja wa Mataifa, UNFPA linafanya kazi nchini humo kupunguza matukio hayo na madhara yatokanayo na utekelezwaji wake hususan ndoa za mapema na ukeketaji.

“Kuendelea kutekelezwa kwa vitendo hivi hatari kunahusishwa na mila, tamaduni na imani,” amesema Edwige Adekambi Domingo, Mwakilishi mkazi wa UNFPA nchini Chad akisema kuwa vitendo hivi vinawekea  ukomo uwezo wa wanawake na wasichana barubaru na vinaongeza hatari yao ya kutumbukia kwenye umaskini na ubaguzi zaidi.

Hata hivyo kuna mabadiliko. Kampeni ya  kina ya uchechemuzi iliyoandaliwa na UNFPA kwa ushirikiano na viongozi wa kidini wakiwemo wale wa dini ya kiislamu na chama cha wanawake waumini wa dini ya kiislamu. Kampeni hii inashinikiza bunge kupiga kura kuunga mkono sheria ambayo inaridhia amri ya rais ya kupiga marufuku ndoa za umri mdogo na kuweka umri wa mtu kuoa au kuolewa kuwa miaka 18.

Hata hivyo, ndoa za mapema na ngono isiyo ya maridhiano bado vinafanyika. “Umaskini ukichanganywa na wanawake kujiona kuwa hawana thamani kwenye jamii, viwango vikubwa vya uzazi na kiwango kidogo cha elimu miongoni mwa watoto wa kike ndio sababu kuu,” amesema Edwige Adekambi Domingo, mwakilishi wa UNFPA nchini Chad.

Anasema  “UNFPA imeazimia kuongeza fursa za kupatikana kwa huduma za afya ya uzazi zilizo bora na rafiki kwa vijana nchini Chad ili wasichana barubaru waweze kufikia huduma hizo bila kikwao, ikiwemo wale ambao wako hatarini kuozwa mapema,” amesema Bi. Domingo.

 

 

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter