Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajabu jimbo moja la Syria linadhibitiwa na magaidi- Ripoti

Watoto wakiwa katika hema wanalolitumia kama darasa katika kambi ya wakimbizi ya Junaina kaskazini mwa Idlib, Syria.
UNICEF/UN0248439/Watad
Watoto wakiwa katika hema wanalolitumia kama darasa katika kambi ya wakimbizi ya Junaina kaskazini mwa Idlib, Syria.

Ajabu jimbo moja la Syria linadhibitiwa na magaidi- Ripoti

Amani na Usalama

Ripoti ya 17 kuhusu hali ya kibinadamu nchini Syria imesema licha ya kupungua kwa chuki nchini humo, bado  ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria vimeendelea kusababisha machungu kwa raia.

Ripoti hiyo yenye kurasa 20 imewasilishwa leo mjini Geneva, Uswisi na Mwenyekiti wa Tume huru ya kimataifa ya uchunguzi kuhusu Syria, Paulo Pinheiro.

Kwa kina ripoti hiyo inaweka bayana ni kwa jinsi gani matukio ya ukiukwaji wa haki yanasababisha hata wasyria waliokimbia nchini humo wahofie kurejea nyumbani sambamba na wale walio wakimbizi wa ndani kushindwa kurejea kwenye maeneo yao ya awali.

Mathalani ripoti imesema kati ya mwezi Julai 2018 na mwezi Januari mwaka huu, mapigano makali yameendleea kaskazini-magharibi na mashariki mwa Syria huku raia wakibeba mzigo wa zahma hiyo.

Vitendo vya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu vimeripotiwa ikiwemo mashambulizi yanayolenga raia, kushambulia maeneo muhimu na mateso, vitendo ambavyo vinafanywa na vikundi vilivyojihami.

Bwana Pinhero ametaja pia mashambulizi yanayofanywa na vikundi vinavyounga mkono serikali na washirika huko Dayr al-Zawr na kusababisha mateso kwa raia na zaidi ya yote..

“Raia wapatao milioni 3 wanaohaha bado wanaendelea kuvumimilia kwa machungu kwenye jimbo la Idlib chini ya utawala kandamizi wa magaidi wa Al Shant ambao kwa kiasi kikubwa wanadhibiti jimbo hilo. Ni jambo la ajabu na kweli kwamba kundi la kigaidi linadhibiti moja ya majimbo ya Syria.”

Mwenyekiti huyo wa kamisheni kuhusu Syria amesema kinachotia hofu zaidi ni kwamba hakuna kabisa utashi wa kisiasa wa kuleta pamoja pande kinzani ili hatimaye kupatikane suluhu ya kisiasa na wakimbizi wa ndani na wa nje waweze kurejea nyumbani.

Kwa mantiki hiyo amesema yeyé na makamishna wenzake..

“Sasa kuliko wakati wowote ule tunasisitiza maendeleo ya dhati kwenye mchakato wa kisaisa unaoweza kuleta pamoja pande kinzani pamoja ili wajadili mustakabali wa Syria.”
 

Tume hiyo yenye wajumbe watatu akiwemo mwenyekiti Paulo Sérgio Pinheiro ilianzishwa na Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ili kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye taifa hilo ambalo mzozo wake ulianza machi 2011.

Ripoti hiyo ingawa imezinduliwa leo, itawasilishwa mbele ya Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa tarehe 12 mwezi ujao.