Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu  haiwezi kusubiri wapeleka nuru kwa watoto CAR

Jospin (katikati) mkimbizi wa ndani wakiwa kwenye darasa linaloendelshwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, CAR, MINUSCA.
UNICEF/UN0149422/Sokhin
Jospin (katikati) mkimbizi wa ndani wakiwa kwenye darasa linaloendelshwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, CAR, MINUSCA.

Elimu  haiwezi kusubiri wapeleka nuru kwa watoto CAR

Utamaduni na Elimu

Serikali ya Jamhuri  ya Afrika ya Kati, CAR kwa ushirikiano na mradi wa Elimu haiwezi kusubiri, ECW,  leo wamezindua mradi wa miaka mitatu wenye lengo la kuboresha elimu nchini humo kama njia mojawapo ya kunasua watoto wa kike na wa kiume kutoka athari za mzozo ulioacha karibu watoto 500,000 bila ya shule.

Taarifa iliyotolewa leo na pande mbili hizo kwenye mji mkuu wa CAR, Bangui, imesema mradi huo unalenga kufikia watoto 900,000 ambapo nusu yao ni wasichana.

Elimu ndio ufunguo wa kila kitu

“Elimu itajenga msingi wa amani, usalama na maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa CAR,” amesema Aboubakar Moukadas-Noure, Waziri wa Elimu wa taifa hilo ambalo tangu mwaka 2012 lilikuwa limegubikwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Amesema kwa kuwapatia wasichana na wavulama pahala salama pa kujifunzia, walimu wabobezi, vifaa vya kujifunzia, mlo shuleni ana huduma za nasaha, mradi huo unafungua ukurasa mpya kwa maendeleo ya Jamhuri ya Afrika ya  Kati.

“Watoto wetu wanastahili kupata elimu. Na iwapo tunaweza kutokomeza njaa, ghasia na ukimbizi wa ndani pamoja na umaskini nchini mwetu, basi elimu haitaweza kusubiri,” amesema Waziri huyo wa elimu.

Mradi wa Elimu Haiwezi Kusubiri

Mradi huo unajinufaisha na uwekezaji wa awali wa dola milioni 6.5 kwa kipindi cha mwaka 2019/2020 kutoka mradi wa Elimu haiwezi Kusubiri, ECW ambao ni mradi mpya wenye lengo la kunasua waliokumbwa na janga la elimu.

ECW  imeahidi kutoa nyongeza ya dola milioni 6.5 kila mwaka kwa kipindi cha mwaka wa pili na wa tatu wa mradi huo kwa kuzingatia mafanikio ya miaka miwili ya 2019/2020.

Mshauri mwandamizi wa ECW, Graham Lang akizungumzia hatua hiyo ya leo amesema “jamii ya kimataifa inapaswa kuongeza jitihada zake kuchukua hatua kwa ajili ya sekta ya elimu CAR. Changamoto zinazokabili watoto nchini hukmo za kupata elimu bora ni kubwa. Hata hivyo mnepo wa watoto hawa ni mkubwa kuliko.”

Amesisitiza kuwa elimu ndio ufunguo ambao utaweza kuwainua na kuwawezesha kufikia ustawi wao wa juu zaidi na wawe waleta mabadiliko, akisema, “bila elimu, hakutakuwepo na kujikwamua endelevu, maridhiano na amani.”

Mambo ya msingi ya mradi huo wa ECW

  • Kutakuwepo madarasa ya mpito, vyumba zaidi  ya 1000 vya madarasa vitajengwa na vikasha zaidi ya 320,000 vyenye vifaa vya shule vitagaiwa.
  • Lengo ni kufikia watoto 320,000 wasio shuleni ili wawepo kwenye mazingira salama ya shule ili  hatimaye asilimia 90 ya wanafunzi nchini humo wawe kwenye mfumo rasmi wa shule.
  • Nchini CAR mtoto mmoja wa kike kati ya wanne ndiye anayefahamu kusoma na kuandika ambapo mradi huu mpya  unalengo la kuongeza kwa asilimia 5 idadi ya watoto wa kike walio katika mfumo rasmi au usio rasmi wa elimu.
  • Halikadhalika mradi  utasaidia wasichana na wavulana 90,000 kupata nyaraka rasmi.