Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hongera kwa miaka 100 ya siku ya kuzaliwa Brian Urquhart- Umetendea mema UN

Brian Urquhart, mmoja wa wafanyakazi wa kwanza kabisa wa Umoja wa Mataifa, amehudumu chini ya makatibu wakuu kadhaa wa UN ambapo wadhifa wake wa mwisho kabla ya kustaafu ilikuwa Msaidizi wa Katibu Mkuu masuala ya siasa.
UN /Mark Garten
Brian Urquhart, mmoja wa wafanyakazi wa kwanza kabisa wa Umoja wa Mataifa, amehudumu chini ya makatibu wakuu kadhaa wa UN ambapo wadhifa wake wa mwisho kabla ya kustaafu ilikuwa Msaidizi wa Katibu Mkuu masuala ya siasa.

Hongera kwa miaka 100 ya siku ya kuzaliwa Brian Urquhart- Umetendea mema UN

Masuala ya UM

Ikiwa leo ni miaka 100 tangu kuzaliwa Sir. Brian Urquhart, mmoja wa wafanyakazi waanzilishi zaidi wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu Antonio Guterres ameumwagia sifa lukuki ikiwemo utumishi uliotukuka na uliosaidia kujenga misingi ya chombo hicho kilichoundw mwaka 1945 baada ya Vita Vikuu vya Pili vya dunia.

Katika ujumbe wake wa siku hiyo hii leo, Katibu Mkuu Guterres amesema, “naungana na makundi mengi ya wavutiwa wa Sir Brian kote ulimwenguni katika kumtakia heri ya miaka 100 ya kuzaliwa ya mfanyakazi gwiji wa muda mrefu wa Umoja wa Mataifa.”

Ameendelea kusema kuwa alama alizoacha Sir Brian kwenye Umoja wa Mataifa ni za kina kama ilivyo kwa mtu yeyote ile kwenye historia ya chombo hicho ambacho sasa kina wachama 193.

Sir Brian ni misingi ya utumishi unaozingatia kanuni

“Akiwa mmoja wa wafanyakazi wa mwanzoni kabisa, aliweka viwango vya watumishi wa umma wa kimataifa: wanaofuata kanuni, wanaojituma na wasiogemea upande wowote,” amesema Katibu Mkuu Guterres.

Halikadhalika amesema akiwa msaidizi wa Katibu Mkuu Dag Hammarskjöld, Sir Brian alisaidia kuainisha wigo wa hatua za Umoja wa Mataifa katika kushughulikia mizozo na changamoto nyingine duniani.

“Na akiwa mshirika wa karibu wa Ralph Bunche, mtendaji mwingine wa aina yake, Sir Brian alisaidia kuanzisha na kusongesha operesheni za kimataifa za ulinzi wa amani kwa kutumia bendera ya Umoja wa Mataifa,” ameendelea Katibu Mkuu katika sifa zake kwa Sir. Brian.

Chimbuko la Sir Brian na kusongesha amani

Bwana Guterres ametanabaisha kuwa ari ya Sir Brian katika kusaka amani ilichagizwa na ushiriki wake katika Vita Vikuu vya Pili vya dunia ambako alikuwa ni miongoni mwa askari wa ushirika waliokuwepo punde tu baada ya kukombolewa kwa kambi ya kifo ya Bergen-Belsen.

Hata hivyo amesema miongo kadhaa, huduma za Sir Brian kwa makatibu wakuu waliomtangulia Guterres, imekuwa kitovu cha matukio yanayobadilisha dunia kuanzia Congo hadi Mashariki ya Kati.

Sir Brian Urquhart looks back to the creation of the UN

Katibu Mkuu amesihi mtu yeyote mwenye nia ya kufanya kazi na Umoja wa Mataifa au mwenye nia ya kufahamu kazi za Umoja wa Mataifa asome kitabu A Life in Peace and  War, au Maisha wakati wa amani na vita, kilichoandikwa na Sir Brian.

Sir Brian anatambuliwa pia kwa maandiko kadhaa ya matukio mbalimbali kupitia mtazamo wake ikiwemo Mobutu na Tshombe, viongozi wa DRC waliotwamisha nchi yao na Mfahamu Patrice Lumumba kupitia simulizi ya Brian Urquhart wa UM.

Bwana Guterres amesifu pia mtazamo wa kuwa na matumaini wa Sir Brian akisema umesaidia kwenye muundo wa Umoja wa Mataifa sambamba na yeye mwenye Sir Brian.

“Tunapoadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwake, tunashukuru sana kwa mchango wake wa kipekee usiolinganishika akiwa ni mtumishi wa Umoja wa Mataifa,” ametamatisha Katibu Mkuu.