Wanawake wavunja mwiko Rwanda, waingia kwenye uvuvi; Maisha yabadilika

26 Februari 2019

Nchini Rwanda kile ambacho awali kilionekana kuwa ni mwiko, wanawake kuwa wavuvi hivi sasa kimekuwa ni jambo la kawaida na linasaidia kutokomeza umaskini katika wilaya ya Rusizi nchini humo.

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO kupitia makala iliyochapishwa kwenye wavuti wake linasema kuwa miaka miwili iliyopita isingaliwezekana kabisa kutaja maneno wanawake na uvuvi kwa fikra potofu kwamba uvuvi si jukumu la wanawake.

Hata hivyo hivi sasa wanawake wamekumbatia kazi hiyo hususan wakazi wa kisiwa cha Nkombo kilichoko kwenye ziwa Kivu wilayani Rusizi jimbo la Magharibi nchini Rwanda.

Miongoni mwao ni Valeria Maniraguha, mwenye umri wa miaka 38. Akiwa ni mama wa watoto wanne, Valieria alianza uvuvi mwaka 2010 ambapo kabla ya kujitumbukiza kwenye kazi hii alikuwa ni mchuuzi wa samaki, stadi ambayo hata hivyo hivi sasa inamsaidia sana pindi anapouza samaki aliovua.

 “Nilivutiwa sana na samaki kwa sababu niliona wavuvi wakipata fedha nyingi zaidi kuliko sisi. Siku moja nilijaribu uvuvi, na watu waliniunga mkono. Walinisaidia kuvuta dau lenye samaki, lakini wakati mwingine nilikataa wasinisaidie kwasababu nilitaka nijifunze mwenyewe,” amesema Valerie.

Mumewe Valeria ambaye anafanya kazi ya ulinzi usiku kwenye duka la dawa la wilaya ya Rusizi, anaunga mkono uamuzi wa mkewe kuwa mvuvi ambapo Valerie anasema, “mume wangu haoni vibaya kabisa. Ni kwamba  yeye mwenyewe alikuwa mvuvi kwa hiyo nilimueleza kuwa nimependa kufanya kitu kipya na hakuwa na shaka kabisa.”

KUIMARISHA STADI MPYA

Saa nane alfajiri, Valeria na kundi la wanawake 10 wanakwenda kuvua samaki. Kila mtu ana jukumu la kufanya: kushikilia taa, kutupa nyavu majini na wengine kuvuta nyavu zenye samaki na kuziingiza kwenye dau.

Wanavua dagaa ambao wanajulikana kama Isambaza, na aina nyingine ya samaki kama vile, Ndugu na Isamake, ambao wanauza kupitia chama chao cha ushirika kiitwacho “Dushakumurimo,” ambacho kinajumuisha wachuuzi wa samaki wanawake na wanaume kutoke ziwa Kivu. Beseni moja la Isambaza, sawa na kilo 15  huuzwa kwa takribani dola 26.

 “Tunaweza kuvua kati ya kilo 15 hadi 150 za samaki ndani ya saa 3 kulingana na aina ya samaki,” amesema Valeria akiongeza kuwa kwa kutumia madau haya ya kupiga kwa makasia inachukua dakika 40 kusafirisha samaki kutoka majini hadi nchi kavu huko wilaya ya Kamembe.

UN News/Dan Dickinson
Mvuvi Falmata Mboh Ali (kulia) akiwa na mwenzake kwenye ziwa Chad wakisaka samaki ambao idadi yao imepungua kutokana na kusinyaa kwa ukubwa awa ziwa hilo.

FAO YASIKIA KILIO CHA WAVUVI

Dushakumurimo na vyama vingine vitatu wilayani Rusizi, hivi karibuni vilipata msaada wa madau ya kutumia mota kutoka FAO.

Madau haya yanasaidia wavuvi kufanya kazi yao kwa tija zaidi kwa kusafirisha haraka samaki hadi kwa wateja mwaloni.

Pamoja na madau, kila mwanachama amepatiwa kizibau cha kuokoa maisha ili kuzuia kuzama pindi wanapokuwa majini.

 “Haya madau yatatusaidia kuwasilisha samaki wetu haraka na pia kuimarisha kipato chetu na pia kupanua wigo wa wateja wetu,” amesema Valeria.

Mwaka 2015, FAO ilianzia mradi wa vijana na wanawake kwa lengo la kuimarisah fursa za ajira kwa kupanua stadi kwa vijana na wanawake kwenye kazi wanazofanya.

FAO inasema kihistoria, wanawake na vijana nchini Rwanda wamekuwa hawana fursa za ajira na wanafanya kazi katika mazingira magumu lakini sasa Valeria ameazimai kubadili mtazamo huo.

KUBORESHA USALAMA, USAFI NAUHIFADHI WA SAMAKI

Alipoulizwa kuhusu changamoto za uvuvi, Valeria anakiri kuwa uvuvi ni kazi hatarishi sana hasa pindi kunapokuwepo na mvua kubwa na upepo mkali.

 “Mwezi Aprili mwaka 2009 nilimpoteza mvuvi mwenzangu mwanamke. Alizama kwasababu ya  upepo mkali. Iwapo tungalikuwa na vizibau vya uokozi pengine asingalipoteza maisha. Ni vyema kuwa hivi sasa tuna vizibao hivyo,” amesema Valeria.

Hivi sasa Valeria na wenzake wamepata mafunzo ya kuimarisha usalama na usafi wa kushughulikia samaki na zaidi ya yote stadi za kuongeza thamani mathalani kukausha samaki.

KUSAIDIA FAMILIA YAKE

Valeria anakiri kuwa hivi sasa anaweza kusaidia familia yake kwa kuwa anapata kipato cha ziada. Kipato cha mume wake kinatumika kulipia ada za shule za watoto ilihali kipato chake Valeria kinasidia familia kununua aina mbalimbali za chakula.

Siku hizi Valeria anajivunua kuwa anawea kulisha familia yake mlo kamili wa wali, mahindi na mboga za majani na bila shaka samaki.

TAGS: Wavuvi wanawake, Rwanda, Rusizi, FAO

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter