Dunia isilale katika udhibiti wa silaha-Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mkutano wa udhibiti wa silaha uliofanyika Geneva Uswisi 25 Februari 2019
UN /Antoine Tardy
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mkutano wa udhibiti wa silaha uliofanyika Geneva Uswisi 25 Februari 2019

Dunia isilale katika udhibiti wa silaha-Antonio Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres hii leo akihutubia mkutano maalumu unaofanyika mjini Geneva Uswisi kuhusu udhibiti wa silaha amesema maono mapya ya kimataifa ya udhibiti wa silaha yanahitajika na nchi hazipaswi "kulala" katika mbio mpya ya silaha za nyuklia.

Guterres ameeleza kuhusu vitisho kadhaa dhidi ya usalama wa dunia kutokana na kuenea kwa silaha akitolea mfano silaha za kemikali, silaha zinazojiendesha zenyewe na kuweza kushambulia kwa kadri zilivyoelekezwa kwa mfumo wa komputa na pia silaha za masafa marefu.

Maoni ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa yamekuja siku chache kabla ya mkutano wa pili kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Kim Jong-un wa Korea kaskazini.

Guterres amesema, “maelfu ya maisha ya raia yanaendelea kupotea kwasababu ya matumizi haramu ya silaha ndogondogo na matumizi ya silaha za uwanja wa vita katika miji.

Amesema miaka 70 iliyopita imeshuhudia maendeleo makubwa katika juhudi za udhibiti wa silaha, Guterres amesisitiza, akisema kuwa zile zilizofanikiwa zaidi ni zile zilizoongozwa na “nguvu kubwa” lakini mafanikio hayo yako hatari kutokana na aina mpya ya silaha.

Akielezea hatari ya kuruhusu kukoma kwa mkataba wa udhibiti wa silaha uliofikiwa kati ya Marekani na Urusi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Guterres ameonya kuwa nchi za Ulaya zitakuwa miongoni mwa nchi za kwanza ambako ukosefu wa usalam utahisiwa zaidi.

Guterres amesisitiza, “juhudi zinatakiwa kufanyika ili kuongeza mwanzo mpya wa mkataba kati ya Marekani na Urusi kabla haujafika mwisho wake mwaka 2021.