Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya tahadhari Sudan inatia shaka mchakato wa amani- Keita

Bintou Keita, Mkuu wa masuala ya Afrika katika Idara ya operesheni za ulinzi wa amani za UN akihutubia Baraza la Usalama
UN /Loey Felipe
Bintou Keita, Mkuu wa masuala ya Afrika katika Idara ya operesheni za ulinzi wa amani za UN akihutubia Baraza la Usalama

Hali ya tahadhari Sudan inatia shaka mchakato wa amani- Keita

Amani na Usalama

Naibu msaidizi wa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Bintou Keita amesema hali ya dharura iliyotangazwa nchini Sudan na rais wa nchi hiyo, Omar Al-Bashir inatia mashakani zaidi mustakabali wa mchakato wa amani nchini humo ambao tayari  ulishakwama.

Bi. Keita ambaye yuko Idara ya Ulinzi wa amani ya Umoja wa Mataifa akihusika na bara la Afrika, amesema hay oleo wakati akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana jijini New York, Marekani kuangalia hali ya Darfur nchini Sudan.

Ikiwa ni hivi karibuni tu amerejea kutoka ziarani Darfur kupatia msukumo mchakato wa amani, Bi. Keita amesema hali ya dharura imesababisha kuvunjwa kwa serikali kuu na serikali za majimbo huku bunge la kitaifa na yale ya majimbo sambamba na mawaziri wa mambo ya nje, sheria na ulinzi zikisalia na majukumu yao.

Halikadhalika, magavana wapya 18 kutoka jeshini na vyombo vingine vya dola waliteuliwa ili kushika nafasi za magavana waliofukuzwa kazi,

Hata hivyo amesema hadi sasa hawajaweza kutathmini athari za maendeleo ya sasa huko Sudan kwenye mchakato wa amani Darfur, “hata hivyo ubadilishaji wa magavana utakuwa na athari kwenye mchakato na baadhi ya vikundi vya waasi vimeonyesha kushikilia misimamo yao.”

Wakimbizi wa ndani jimbo la Darfur Sudan wanakabiliwa na changamoto nyingi na ugumu wa kupata maji safi. Pichani ni msichana na kaka yake wakiwa katika kituo cha maji safi cha Abu-Shok kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani illi kuteka maji
UNAMID/Mohamad Mahady
Wakimbizi wa ndani jimbo la Darfur Sudan wanakabiliwa na changamoto nyingi na ugumu wa kupata maji safi. Pichani ni msichana na kaka yake wakiwa katika kituo cha maji safi cha Abu-Shok kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani illi kuteka maji

Hata hivyo amesema licha ya hivyo, matukio ya mapigano ya kikabila huko Darfur sambamba na matukio ya kutishia usalama, yamepungua isipokuwa kwenye maeneo machache kama vile Jebel Marra.

 “Eneo la Jebel Marra bado ni ukanda wa mzozo ambapo bado hakuna sitisho la chuki. Kwa ujumla, kuna takribani wakimbizi wa ndani milioni mbili huko Darfur. Kuna umuhimu wa kuimarisha uwezo wa eneo hilo kusimamia masuala ya utawala wa sheria na kuzuia mapigano ya kikabila hususan kule ambako mapigano hayakomi kutokana na mvutano wa masuala ya ardhi, njia za uhamiaji na vyanzo vingine vya mapato,” amesema Bi. Keita.

Amesema bado pia masuala ya haki za binadamu ikiwemo ulinzi wa wanawake n watoto na vijana bado mashakani.

Bi. Keita amekumbusha kuwa pamoja na hali inayoendelea, Umoja wa Mataifa kwa miaka 15 tangu kuanza kwa mzozo huko Darfur, umeweka uwekezaji wa kutosha kwenye Nyanja za kisiasa, kibinadamu na ulinzi wa amani, “kwa hiyo ni jukumu letu la pamoja kuhakikisha kuwa ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muugano wa Afrika, Darfur, UNAMID unapojiandaa kuondoka, hakutasalia ombwe ambalo litasababisha kushamiri kwa ghasia au kuibuka kwa viashiria vipya ya hatari.”