Ukatili dhidi ya watoto waendelea vitani Yemen: UNICEF

Wakati mkutano kuhusu mzozo wa Yemen unaendelea mjini Geneva Uswisi hii leo, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, limetoa wito kwa wadau wote kutoa kipaumbele kwa suala la ulinzi wa watoto na kuheshimu haki zao za msingi.
Wito huu umetokana na ripoti za UNICEF zinazoonyesha kwamba hadi sasa takribani watoto milioni 1.2 wanaendelea kuishi katika maeneo 31 yenye mzozo ikiwemo Hudaydah, Taizz, Hajjah na Sa’da.
Kulingana na Geert Cappelaere, Mkurugenzi UNICEF kanda za Mashariki ya kati na Kaskazini mwa Afrika , maeneo wanamoishi bado yanashuhudia ukatili mkubwa unaoambantana na mapigano makali.
Amesema hamna mabadiliko chanya ya kutosha kuhusiana na hali ya watoto nchini Yemen licha ya kutiwa saini mkataba wa Stockholm tarehe 13 Decemba 2018.
Bwana Cappelaere amefafanua kuwa tangu mkataba huo, angalau watoto 8 wanauawa au kujeruhiwa kila siku wakiwa michezoni majumbani na wengine wakati wa kwenda au kutoka shuleni.
Miaka 4 ya mzozo wa miongo kadhaa nchini Yemen imechochea viwango vya umaskini na kuvunja uthabiti na ustawi miongoni mwa jamii za Wayemen hasa watoto.
Kwa mara nyingine, UNICEF inatoa wito kwa pande zinazohusika na mzozo nchini Yemen kulinda raia vitani na kuruhusu huduma za kibinadamu kufikia watoto na familia zao.
UNICEF pia imeiomba jamii ya kimataifa kutoa michango isiyokuwa na masharti kwa ajili ya kusaidia kuokoa maisha ya watoto na kuwekeza zaidi katika mustakabali nchini humo.