Bila fedha mamilioni ya walio na njaa Yemen watakuwa njia panda:WFP

25 Februari 2019

Wakati mkutano wa kimataifa wa uchangishaji fedha kwa ajili ya Yemen ukifanyika leo mjini Geneva Uswis na kuwaleta pamoja wadau mbalimbali  wa kimataifa na mashirika wahisani, shirika la Umoja wa  Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, limesema linahitaji haraka dola milioni 570 ili kususuru maisha ya mamilioni ya wanaohitaji msaada wa chakula. 

Kwa mujibu wa WFP fedha hizo ni za kulisha watu milioni 12 walio katika hali mbaya zaidi na wasio na uhakika wa chakula kwa miezi sita ijayo. Wayemeni karibu milioni 20 sawa na asilimia 70 ya watu wote hawatokuwa na uhakika wa chakula endapo hawatopokea msaada wa kibinamu  unaotegemea upatikanaji wa fedha hizo.

Katika hospital  hii mjini Haijjah miongoni mwa wanaohitaji msaada huo wa WFP ni mtoto Mouaid Alquattin mwenye umri wa miezi 18 , ambaye uzito wake ni kilo 3 tu akikabiliwa na utapiamlo uliokithiri. Wiki nne zilizopita mama yake Safia  alimleta Worood dada wa Mouaid akiwa na tatizo hilo hilo na baada ya kutibiwa alirejea nyumbani lakini siku chache baadaye akaugua tena na kufariki dunia sasa Safia ana hofu kubwa kwamba mwanae Mouaid pia atafariki dunia kama dada yake

(SAUTI YA SAFIA)

“Alikuwa mgonjwa na siku zote tulijaribu kumtibu. Afya yake ikawa mbaya zaidi na akageuka kutoka ngozi na kuwa mifupa.”

Mwaka huu WFP inalenga kuwalisha watu milioni 12 kwa mwezi ambao wako katika hali mbaya ya chakula ikiwa ni ongezeko la asilimia 50 la malengo ya mwaka 2018. Na inasema kiwango hiki cha usaidizi ni muhimu kuzuia zahma  zaidi. Stephen Anderson ni mkurugenzi wa WFP Yemen

(SAUTI YA STEPHEN ANDERSON)

“Tunafahamu kutokana na tarifa zetu tulizozikusanya mwaka jana kwamba msaada wetu wa chakula kwa hakika ulisaidia kuzuia baa la njaa na katika wilaya nyingi zilizoathirika vibaya uhakika wa chakula umeimarika. Hivyo tunajua kwamba tuko katika mstari sahihi , lakini tunahitaji haraka rasilimali. Mwaka huu pekee tunahitaji dola takriban milioni 1.5”

WFP inaendesha zoezi la usajili nchini Yemen , mchakato ambao tayari umeanza Kusini mwa nchi hiyo na WFP inartarajia kulifanya zoezi hilo Kaskazini mwa nchi miezi michache ijayo ili kuinua kiwango cha uwazi na uwajibikaji. Pia inaendesha kituo cha upokeji simu mjini Sana’a na amman ambacho kinaruhusu watu kutoa malalamiko yao ambapo , na kuripoti ugumu wanaokabiliana nao katika kupokea misaada.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter