Utashi wa kisiasa wahitajika kuleta utulivu wa kudumu Maziwa Makuu- Djinnit

25 Februari 2019

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa nchi za Maziwa Makuu Said Djinnit amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa mkataba wa amani, usalama na ushirikiano, PSC kwa ajili ya Jahmhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na eneo hilo la Maziwa Makuu, bado kuna changamoto za kuweza kuufanikisha kwa kina. 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi, Kenya hii leo, Bwana Djinnit ambaye anatamatisha jukumu hilo tarehe 31 mwezi ujao ametaja mafanikio ya mkataba huo uliotiwa saini mwaka 2013 kuwa ni pamoja na kurejesha makwao wapiganaji wa kigeni ambao walijisalimisha na kupokonywa silaha, mpango ulioanza mwaka 2018.

Amesema pamoja na kurejesha wapiganaji, mpango huo umesaidia kuimarisha ushirikiano baina ya DRC, Rwanda na Uganda kwenye suala hilo la mzozo unaohusisha vikundi vilivyojihami akitolea mfano wapiganaji wa zamani wa kikundi cha FDLR waliojisalimisha ambao wao na wategemezi wao walisafirishwa kutoka DRC na kurejea Rwanda.

Bwana Djinnit amesema hivi sasa harakati zinaendelea ili kufanikisha kurejesha makwao waliokuwa wapiganaji wa M-23.

Hata hivyo amesema licha ya mafanikio hayo bado kuna changamoto kwa kuwa kuna vikundi kama vile ADF ambavyo bado vinatishia usalama wa raia huko Mashariki mwa DRC na hivyo kinachotakiwa ni utashi wa kisiasa miongoni mwa pande husika akisema..

(Sauti ya Said Djinnit)

“Wito wangu ni kwamba viongozi wa eneo hili, wakazi wa Maziwa Makuu waonyeshe ari zaidi katika kuhakikisha wanarejesha utulivu eneo la Maziwa Makuu kwasababu utulivu na maendeleo kwenye Maziwa Makuu vina mchango mkubwa katika utulivu na maendeleo barani Afrika.”

Mkataba wa amani, ulinzi na ushirikiano, PSC kwa ajili ya DRC na ukanda wa Maziwa Makuu, ulitiwa saidni tarehe 24 mwezi Februari mwaka 2013  huko Addis Ababa nchini Ethiopia na mataifa 11 ya Afrika ambayo ni Angola, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Rwanda, Afrika Kusini, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud