Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani 3 wa UN wauawa Mali

Walinda amani kutoka Chad wakipiga doria katika mitaa ya Kidal nchini Mali.(maktaba Desemba 2016)
MINUSMA/Sylvain Liecht
Walinda amani kutoka Chad wakipiga doria katika mitaa ya Kidal nchini Mali.(maktaba Desemba 2016)

Walinda amani 3 wa UN wauawa Mali

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mauaji ya walinda amani watatu wa umoja huo nchini Mali.

Walinda amani hao kutoka Guinea waliuawa kufuatia shambulio lililofanywa dhidi ya msafara wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA kwenye eneo la Siby karibu na mji mkuu wa Mali, Bamako.

Katibu Mkuu kupitia taarifa ya msemaji wake iliyotolewa mjini New York, Marekani ametuma salamu za rambirambi kwa familia za walinda amani hao na serikali ya Guinea huku akiwatakia ahueni ya haraka walinda amani wengine waliojeruhiwa kwenye shambulio hilo la jumamosi.

Huku akieleza mshikamano wake na Guinea, Bwana Guterres ameonya kuwa shambulio lolote dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa linaweza kuwa uhalifu wa kivita.

Ametoa wito kwa mamlaka za Mali ziwasake wahusika wa shambulio hilo na wafikishwe mbele ya sheria.

Bwana Guterres amesisitiza azma ya MINUSMA kuendelea kutekeleza mamlaka yake ya kusaidia wananchi wa Mali katika harakati zao za kusaka amani.