Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bangladesh yachukua hatua kutunza na kuhifadhi lugha za mama

Siku ya mama duniani
UNESCO Photo
Siku ya mama duniani

Bangladesh yachukua hatua kutunza na kuhifadhi lugha za mama

Utamaduni na Elimu

Leo ni siku ya lugha ya mama duniani ambapo Umoja wa Mataifa unapigia chepuo matumizi ya lugha ya mama katika mifumo yote ya maisha iwe elimu, biashara kwa lengo la kuimarisha amani, ustawi na utangamano miongoni mwa watu wenye makabila, lugha na tamaduni tofauti. 

Licha ya umuhimu wa lugha katika kumtambulisha mtu na hata utamaduni wake, Umoja wa Mataifa unatiwa hofu kuwa kutokana na mchakato wa utandawazi lugha mama zinapotea na kila baada ya wiki mbili lugha moja inatoweka kwenye  ulimwenguni huu ambamo lugha 600 za mama ziko hatarini kutoweka.

Bangladesh ambayo ni miongoni mwa mataifa yaliyokuwa mstari wa mbele kupitishwa kwa azimio la siku ya lugha ya mama mwaka 1999 kupitia mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Masud Bin Momen inasema imechukua hatua kulinda lugha hizo..

(Sauti ya Balozi Masud Bin Momen)

« Nchini Bangladesh tumeanzisha kituo cha kimataifa cha lugha za mama kutafiti lugha ambazo zinatoweka na jinsi gani ya kuzitunza. Na nchini kwetu kwenyewe tuna jamii ndogo za asili na mfumo wetu wa elimu umeanzisha mfumo mpya ili watoto wa makabila haya madogo waweze kutumia lugha ya mama wanapoanza masomo kwa mara ya kwanza sambamba na lugha ya taifa Bengali na kiingereza ambacho kinafundishwa shuleni. »

Balozi Momen akazungumzia umuhimu wa kuhifadhi lugha hata zile za makabila madogo kwenye visiwa vidogo..

(Sauti ya Balozi Masud bin Momen)

“Idadi kubwa ya nchi hizo za visiwa vidogo jamii zina idadi ndogo ya watu kama maelfu tu, na wanaweza kuhamishiwa kwenye nchi  nyingine. La hasha! Jamii ya kimataifa na wakazi wa mataifa haya ya visiwa hiki ni kitu ambacho wanajivunia nacho na wanajitambulisha nacho.”

Siku ya lugha ya mama imekuwa ikiadhimishwa tangu mwezi Februari mwaka 2000 kusongesha utofauti wa lugha, tamaduni na lugha mbalimbali kwa kuzingatia kuwa lugha ni chombo thabiti katika kuhifadhi na kuendeleza turathi za tamaduni zisizogusika za kibinadamu.