Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dhamira ipo katika kutekeleza makubaliano ya Stockholm, Yemen-Griffiths

Martin Griffiths (kwenye skrini) akihutubia wajumbe wa Baraza la  Usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video kutoka Amman, Jordan leo Januari 9, 2019
UN /Loey Felipe
Martin Griffiths (kwenye skrini) akihutubia wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video kutoka Amman, Jordan leo Januari 9, 2019

Dhamira ipo katika kutekeleza makubaliano ya Stockholm, Yemen-Griffiths

Msaada wa Kibinadamu

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen, Martin Griffiths leo amehutubia kikao cha Baraza la Usalama kwa njia ya video kuhusu kile alitaja kama hatua chanya katika utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa mjini Stockholm nchini Sweden.

Bwana Griffiths amesema makubaliano hayo yaliyofikiwa mwezi Disemba mwaka jana yalitajwa kama ya kupasua anga yakitoa ishara ya mabadiliko.

Amesema “chini ya uongozi wa Luteni jenerali Michael Lollesgaard, pande husika zimekubali katika hatua ya kwanza kuondoa vikosi vyao kutoka bandari za Saleef na Ras Isa na hatimaye hatua ya pili ni kuondoa vikosi vyao kutoka bandari ya Hudaydah na maeneo muhimu ya mji wa Hudaydah ambao unahusishwa na miundombinu ya misaada ya kibinadamu. Hatua hii itarahisisha kufikia ghala la Red Sea ambalo kama tunavyofahamu kuna shehena kubwa ya nafasi ambayo inasubiri kusambaziwa wananchi wa Yemen.”

Mjumbe huyo amesema “ingawa ukomo wa utekelezaji wa mipango hauzingatiwi, pande mbili kwenye mzozo zimeonyesha dhamira yao ya kutekeleza makubaliano na wamenihakikishia mara kwa mara kuhusu dhamira hiyo.”

Bwana Griffiths ameongeza kwamba anaelewa kuna changamoto lakini, “labda kwa siku moja tunaweza kutiwa moyo badala ya kusikitishwa na changamoto zilizopo na ninatiwa moyo na kumbusho kutoka pande mbili kwangu na wenzangu kwamba hii ni fursa ya kipekee.”

Kwa upande wake Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu, OCHA Mark Lowcock amewasilisha ripoti yake kuhusu mahitaji ya kibinadamu kwa Yemen mwaka 2019 yaliyotolewa na ofisi yake wiki iliyopita.

Saleh, mtoto mwenye  umri wa miezi minne, akiwa amelazwa katika hospitali kuu ya Hudaidah na mama yake Nora. Takribani watoto  500,000 nchini Yemen na wanawake wazazi milioni 2 wako hatarini kufariki dunia kutokana na unyafuzi.
UN OCHA/GILES CLARKE
Saleh, mtoto mwenye umri wa miezi minne, akiwa amelazwa katika hospitali kuu ya Hudaidah na mama yake Nora. Takribani watoto 500,000 nchini Yemen na wanawake wazazi milioni 2 wako hatarini kufariki dunia kutokana na unyafuzi.

Kwa mujibu wa ripoti asilimia 80 ya watu nchini Yemen ikiwa ni sawa na watu milioni 24 wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi.

Aidha watu milioni 20 wanahitaji msaada kufikia chakula ikiwemo watu milioni 10 ambao wako katika hatari ya kukumbwa na njaa.

“Isitoshe watu milioni 20 hawana huduma ya afya na wengine takriban milioni 18 hawana maji safi na huduma ya kujisafi. Na watu milioni 3 ikiwemo Watoto milioni mbili wana utapiamlo uliokithiri huku watu milioni 3.3 wamefurushwa makwao,” amesema Bwana Lowcock.

Mkuu huyo wa OCHA amesema mashirika hayana raslimali za kuendesha shughuli zake na kwamba, bila raslimali toshelezi, operesheni za kibinadamu zitafika mwisho wakati ambapo watu wengi zaidi wanahitaji msaada kuliko awali.

OCHA imesema mashirika ya kibinadamu yanalenga kusasidia watu milioni 15 kote nchini mwaka 2019, ikiwemo watu milioni 12 ambao watahitaji msaada wa dharurua wa chakula kila mwezi.

Naye mwakilishi wa kudumu wa Yemen kwenye Umoja wa Mataifa, Abdullah Al-Saadi amesema serikali yake iko tayari kutekeleza makubaliano ya Stockholm na hivyo ameuomba Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kutekeleza wajibu wake katika kufuatilia utkelezaji wa makubaliano hayo.

Mapema leo Umoja wa Mataifa na wadau wake wa misaada ya kibnadamu wametoa ombi la dola bilioni 4.2 kwa ajili ya kusaidia watu milioni 19 nchini Yemen.