Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Basi la aina yake latoa fursa kwa watoto kuwa watoto

Mtoto mkimbizi wa Syria akiwa nje ya hema kwenye kambi yao nchini Lebanon
UNICEF/Alessio Romenzi
Mtoto mkimbizi wa Syria akiwa nje ya hema kwenye kambi yao nchini Lebanon

Basi la aina yake latoa fursa kwa watoto kuwa watoto

Wahamiaji na Wakimbizi

Mjini Beirut, nchini Lebanon, basi la aina yake linarandaranda kwenye mitaa ya mji huo likileta furaha, elimu na matumaini kwa watoto wanaofanya kazi mitaani.

Katika moja  ya mitaa ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut, basi maalum likiwa limeandikwa maandishi makubwa , “basi la furaha” limesimama na watoto wanakimbilia kulipanda. Mmoja wao ni Abed, mkimbizi kutoka Syria…

Anasema wanatuita hapa na kisha wanatuambia njooni mcheze!

Ndani ya basi hili ambalo ni mradi wa pamoja wa shirika la kuhudumia wakimbizi duniani,  UNHCR, Muungano wa Ulaya, EU na taasisi ya  Makhzoumi kuna michezo na vifaa mbalimbali vya kujifunzia.

Hapa watoto wanapata fursa ya kuwa tena watoto, wanaimba… na wanajifunza kuandika herufi kama vile B. Alaa ni mkimbizi pia kutoka Syria..

Anasema alikuwa darasa la 4 baba yake alipofariki dunia na hivyo alilazimika kufanya kazi ya uchuuzi mtaani.

Nchini Lebanon, zaidi ya theluthi moja ya ni hohehahe na hivyo familia zinalazimika kutumbukiza watoto wao kwenye ajira, hivyo Sirine Comati, ambaye ni afisa mwandamizi wa ulinzi wa mtoto UNHCR anasema kupitia basi hili, “si tu tunafanya kazi na watoto, bali pia tunashirikiana na wazazi ili wafahamu hatari za watoto wao kuwepo mitaani.”

Lengo la basi hili ni kupunguza muda wa watoto kuwepo mitaani na hatimaye watoto waweze kuandikishwa shuleni na hadi sasa kupitia basi hili watoto 150 wameondoka mitaani.