UN-Habitat kupata dola laki 7 kutoka Japan kusaidia wanaorejea Darfur Kusini, Sudan.

18 Februari 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la makazi UN-HABITAT mjini Khartoum nchini Sudan limetangaza kuwa Japan imeahidi mchango wa dola laki 7 kwa ajili ya mradi wa kusaidia wakimbizi wa ndani wanaorejea katika eneo la Alsalam, Darfur kusini nchini humo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Machi  mwaka huu hadi Machi mwakani.

Mradi huu utawanufaisha watu 17,100 waliorejea na pia jamii za wenyeji katika kijiji vya Dagariss kilichoko kilomita 22 kusini magharibi mwa Nyala ambao ni  mji mkuu wa Darful Kusini.

Kijiji cha Dagariss ni moja ya jamii ambazo zimeshuhudia idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani wanaorejea Darful. Hata hivyo wanakabiliwa na hali mbaya na uhaba wa huduma muhimu, usalama na wako katika uhitaji mkubwa.

Kupitia msaada huo wa Japan, mradi unalenga kusaidia urejeaji endelevu wa wakimbizi wa ndani na kuhakikisha usalama kwa pande zote yaani wanaorejea na wenyeji hasa katik suala la haki ya ardhi.

Mradi huu unafuatia maamuzi ya Baraza la Usalama yaliyofikiwa Julai 2018 hususani ibara ya 46 inayozungumzia umuhimu wa kukabiliana na masuala ya ardhi kwa ajili ya suluhu ya kudumu katika eneo la Darfur na kuweka mazingira safi ya kuruhusu wakimbizi wa ndani kurejea.

Mwaka uliopita, 2018, Japan iliipatia UN-Habitat kiasi cha dola laki 9 kuwasaidia wakimbizi wa Sudan Kusini na jamii za wenyeji katika eneo la Aljabalain nchini Sudan.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter