Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkataba wa amani CAR waleta matumaini kwa mamilioni ya watoto- UNICEF

Jospin (katikati) mkimbizi wa ndani wakiwa kwenye darasa linaloendelshwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, CAR, MINUSCA.
UNICEF/UN0149422/Sokhin
Jospin (katikati) mkimbizi wa ndani wakiwa kwenye darasa linaloendelshwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, CAR, MINUSCA.

Mkataba wa amani CAR waleta matumaini kwa mamilioni ya watoto- UNICEF

Amani na Usalama

Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF limesema mkataba wa amani uliotiwa saini kati ya serikali na pande kinzani  nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR unaleta matumaini kwa mamilioni ya watoto kwenye taifa hilo lililokuwa limegubikwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore kupitia taarifa iliyotolewa leo mjini New York, Marekani na Bangui CAR amesema utiaji saini huo ni hatua ya mbele kuelekea amani  ya kudumu na matumaini ya mustakabali bora kwa watoto.

“Tunakaribisha hasa hasa ahadi za kulinda haki za watoto na kumaliza ukiukwaji wa kutishi wa haki za watoto, lakini ahadi hizo pekee hazitoshi sasa ni wakati wa kuchukua hatua,” amesema Bi. Fore.

Amesema kwa muda mrefu, ghasia, ukosefu wa utulivu na kudumaa kwa shughuli za maendeleo kumesambaratisha maisha ya watoto nchini CAR.

Amefafanua kuwa theluthi mbili ya watoto nchini humo wanahitaji msaada wa kibinadamu, na mtoto mmoja kati ya wanne amefurushwa makwao au ni mkimbizi, mamilioni hawako shuleni, wana utapiliamlo huku magonjwa yakiwanyemelea bila kusahau manyanyaso na ukatili.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNICEF ametaja hatua madhubuti ambazo zinaweza kusaidia kutafsiri mkataba huo kutoka kwenye maneno kuwa vitendo, kuwa ni pamoja na pande zote kuchukua hatua na kuachilia  huru watoto wote wanaohusishwa na vikundi vilivyojihami.

 Pili mfumo wa mahakama uhakikishe watoto waliokamatwa au kushikiliwa kwa kuhusishwa na vikundi vilivyojihami wanatendewa kama watoto na haki zao zilindwe.
 Hatua ya tatu ni serikali ya CAR ichagize mchakato wa kupitisha kanuni za ulinzi wa mtoto sambamba na mfumo wa mahakama ya watoto unaoendana na viwango vya kimataifa.
 
Amesema UNICEF kwa upande wake iko tayari kusaidia watoto walioathiriwa na vita.