Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wapalestina wameteseka kwa muda mrefu mataifa mawili ndio suluhu pekee-Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres
UN /Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

Wapalestina wameteseka kwa muda mrefu mataifa mawili ndio suluhu pekee-Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amesema wapalestina wamevumilia kwa muda mrefu ikiwa ni zaidi ya nusu karne ya maeneo yao kukaliwa na kunyimwa haki yao ya kujitawala akiongeza kuwa na hadi sasa wanaendelea kuteseka kutokana na msururu wa vikwazo na ukatili.

Akizungumza katika mkutano wa kwanza wa 2019 wa kamati kuhusu haki za watu wa Palestina, Bwana Guterres amesema suluhu ya amani na yenye haki kwa suala la watu wa Palestina inaweza kupatikana kwa uwepo wa mataifa mawili, Israeli na Palestina, wakiishi upande moja na mwingine kwa amani na Jerusalem ikiwa mji mkuu wa mataifa yote mawili. Ameelezea wasiwasi wake kuwa katika kipindi cha mwaka mmojauliopita mwelekeo umekuwa tofauti.

Katibu Mkuu huyo amesisitiza kwamba viongozi wanawajibu kwa wananchi wake, “hata vijana kubadili taswira ya sasa na kuweka njia kwa ajili ya amani, uthabiti na maridhiano.”

Guterres akizungumzia hali Gaza ametoa wito kwa mamlaka wa Hamas kuepukana na chokochoko na kuzingatia kuwa Israeli ina wajibu chini ya sheria za kimataifa kujizuia na kutotumia nguvu kupita kiasi, kando tu na kama ilivyoorodheshwa kwenye sheria za kimataifa kama hatua ya mwisho inapotokea kuna tishio la kifo au majeraha makubwa.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametanabaisha vurugu kwenye Ukingo wa Magharibi akisema, ujenzi na mipango ya makazi na Israeli katika eneo la Area c ikiwemo mashariki wa Jerusalem. Bwana Guterres ameongeza kuwa makazi ni ukiukwaji wa haki za kimataifa kisheria na kwamba yanaeneza kutoaminiana na kuathiri juhudi za suluhu la mataifa mawili akiongeza kuwa ukatili wa wakazi unatia wasiwasi mkubwa.

Guterres amesema hakuna suluhu nyingine kando na la mataifa mawili yanayoishi kwa amani na usalama akiongeza kuwa hiyo ndio njia pekee ya kuhakikisha haki kwa watu wa Palestina.