Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano kati ya UN na AU kuhusu amani na usalama wafanyika Addis Ababa.

Katika picha hii ya maktaba anaonekana Katibu Mkuu wa UN António Guterres akiwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Moussa Faki,  mjini Addis Ababa, Ethiopia. Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika AU wameaidiana kuendeleza ushirikiano katika mambo mbalimbal
UN /Antonio Fiorente
Katika picha hii ya maktaba anaonekana Katibu Mkuu wa UN António Guterres akiwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Moussa Faki, mjini Addis Ababa, Ethiopia. Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika AU wameaidiana kuendeleza ushirikiano katika mambo mbalimbali yakiwemo ya amani na usalama.

Mkutano kati ya UN na AU kuhusu amani na usalama wafanyika Addis Ababa.

Amani na Usalama

Kikosi kazi cha pamoja cha amani na usalama kati ya Umoja wa Mataifa na muungano wa Afrika, AU kimefanya mkutano wake wa sita katika makao makuu ya Muungano wa Afrika mjini Addis-Ababa. 

Kamisheni ya Muungano wa Afrika na sekretarieti ya Umoja wa Mataifa wamewakilishwa na makamishina, Smaïl Chergui (amani na usalama), Minata Samaté-Cessouma (masuala ya siasa), Rosemary DiCarlo (masuala ya siasa na amani), Jean-Pierre Lacroix (operesheni za amani) na Hanna Tetteh (mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Muungano wa Afrika). Waliambatana na maafisa wa ngazi za juu kutoka pande zote mbili wakiwemo  Bience Gawanas mshauri maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika.

Mkutano huo umejadili mambo kadha ikiwemo kutathimini uhusiano kati ya AU na Umoja wa Mataifa, hali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, Afrika ya Kati CAR, Burundi, Mali na ukanda wa Sahel ikiwemo hali ya usalama ya Burkina Faso na Niger. Aidha wamebadilishana mawazo kuhusu hali ya nchini Libya, Sudan Kusini na eneo la bonde la ziwa Chad.

Katika kutathimi hali ya utekelezaji wa masuala kadha kati ya Umoja wa Mataifa na Muuungano wa Afrika hasa katika suala la amani na usalama, kikosi kazi kimekaribisha ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika Madagascar na CAR. Mkutano huo umetambua kuongezeka shughuli za pamoja za operesheni barani Afrika.

Kuhusu Jamhuri ya Afrika ya kati, mkutano umepokea utiwaji saini wa mkataba wa amani na maelewano uliofikiwa mwezi huu wa Februari tarehe 6, 2019.

Kwa upande wa maziwa makuu, wamepongeza uchaguzi wa amani na makabidhiano ya madaraka nchini Jamhuri ya kidemkorasia ya Congo, DRC. Wamepongeza pia utayari wa DRC kushirikiana na Umoja wa Mataifa kutatua changamoto zinazoikabili nchi hiyo. Na kuhusu Burundi wametambua mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Arusha Tanzania tarehe mosi Februrai 2019 na wakarudia ahadi yao ya kuiunga mkono jumuiya ya Afrika mashariki katika usuluhishi.

Mkutano mwingine wa kikosi kazi utafanyika mjini New York mwezi Septemba 2019 kandoni mwa vikao vya baraza kuu la Umoja wa Mataifa.