Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila rasilimali za kutosha WFP haiwezi kufikia watoto ambao maisha yao yako hatarini Yemen

Muhudumu wa afya katika hospitali ya Al Thawra mjini Hudaidah akimchunguza mtoto anayetibiwa kutokana na utapiamlo mkali.
UNICEF/Ahmed Abdulhaleem
Muhudumu wa afya katika hospitali ya Al Thawra mjini Hudaidah akimchunguza mtoto anayetibiwa kutokana na utapiamlo mkali.

Bila rasilimali za kutosha WFP haiwezi kufikia watoto ambao maisha yao yako hatarini Yemen

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP limesema licha ya mpango wake wa dharura wa kusambaza chakula nchini Yemen kuwa mkubwa zaidi kuliko yote duniani ukilenga kila mwezi kuwalisha watu milioni 12 wenye njaa kali na walioko hatarini zaidi, bado takribani watu milioni 16 nchini humo wanahaha kupata mlo kila siku kutokana na uhaba wa chakula. 

Katika hospitali ya Al Thawra mjini Hudaidah nchini Yemen, wanawake wakiwa na watoto wao katika moja ya wodi ya hospitali hiyo. Watoto wameathirika sana na utapiamlo.

WFP inasema zaidi ya watoto milioni 2 nchini Yemen wana utapiamlo na watoto 360,000 kati yao wana utapiamlo mkali zaidi au unyafuzi. Halikadhalika wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wapatao milioni 1.1 nao wana utapiamlo.

WFP inasema mtoto mmoja kati ya watoto watatu na mjamzito mmoja kati ya wajawazito watano na wanawake wanaonyonyesha wanakabiliwa na utapiamlo mkubwa.

Mtaalamu wa Lishe wa WFP, Trust Mlambo, anasema,“Kwanza kabisa, ninafikiri tutakuwa na vifo vya watoto hawa bila sababu yoyote ya msingi. Katika siku za usoni unaweza kutegemea utendaji duni wa watoto hawa ambao watakuwa wamekua bila lishe ifaayo katika miiili yao. Kwa hivyo ni muhimu kuwalinda na kuwaokoa watoto hawa.”

WFP inasema kutokana na utapiamlo, nusu ya watoto wa Yemen wamedumaa kutokana na utapiamlo mkali na kasi ya wanaodumaa imeongezeka kwa asilimia moja kwa mwaka tangu kuanza kwa mgogoro.

Abdul Rahman ni mmoja wa wazazi,“Kwa sababu ya vita hakuna usafiri, hakuna huduma yoyote ya afya. Ni utapiamlo kila wakati. Ni kama baa la njaa kila mahali. Watoto kote nchini wanaumwa”