Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dau la plastiki ladhihirisha #BahariSalama yawezekana

Dau lililotengenezwa kwa taka za plastiki ikiwemo kandambili chakavu. Linafanya safari sasa kutoka Lamu Mombasa nchini Kenya hadi Mji Mkongwe Zanzibar nchini Tanzania
@Flipflopi Project
Dau lililotengenezwa kwa taka za plastiki ikiwemo kandambili chakavu. Linafanya safari sasa kutoka Lamu Mombasa nchini Kenya hadi Mji Mkongwe Zanzibar nchini Tanzania

Dau la plastiki ladhihirisha #BahariSalama yawezekana

Tabianchi na mazingira

Baada ya siku 14 za kupasua mawimbi kwenye bahari ya Hindi kutoka Kenya hadi Tanzania, hatimaye dau lililotengenezwa kwa taka za plastiki lilitia nanga Mji Mkongwe huko kisiwani  Unguja, Zanzibar Tanzania tarehe 7 mwezi Februari kwa mafanikio makubwa.

Safari hiyo ya kilometa 500 kwa lengo la kuchagiza bahari salama au #CleanSeas  na matumizi ya zaidi ya mara moja ya plastiki ilikuwa ni ya mafanikio kwa kuwa ilibadili mtazamo kuhusu matumizi ya plastiki miongoni mwa miji ambapo dau hilo lilitia nanga.

Tani 10 za taka za plastiki  zilizotumika kutengeneza Flipflopi yenye urefu wa mita 9 ni pamoja na kandambili chakavu ambazo ziliokotwa kwenye fukwe na miji ya Kenya na safari yake ilikuwa ni kichocheo kikubwa na simulizi dhahiri ya jinsi ya kukabiliana na changamoto kubwa inayokumba dunia hivi sasa; uchafuzi utokanao na taka za plastiki.

Safari ilianzia Lamu, na kupitia Kipini, Malindi,Watamu, Kilifi, Mombasa, Diani, Shimoni, Wete, Pemba Kusini, Nungwi hadi Mji Mkongwe Zanzibar.

Mwanzoni mwa safari mjini Lamu, Ben Morison ambaye ni mwanzilishi mwenza wa mradi wa Flipflopi akaweka bayana kuwa, “kumbuka safari hii si kwa ajili ya dau tu, tulitaka kuonyesha kuwa matumizi ya mara moja ya plastiki hayana maana yoyote. Tunatarajia watu duniani kote watahamasika na kusaka mbinu zao za kuchukua hatua na kutumia tena na tena plastiki ambazo wametumia.

 

Mwanafunzi akifuatilia kwa makini na kuandika kwenye daftari lake wakati wa warsha huko Diani kandoni mwa ziara ya dau la Flipflopo lililotengenezwa kwa taka za plastiki.
Flipflopi/FinneganFlint
Mwanafunzi akifuatilia kwa makini na kuandika kwenye daftari lake wakati wa warsha huko Diani kandoni mwa ziara ya dau la Flipflopo lililotengenezwa kwa taka za plastiki.

Njiani warsha zilifanyika mfano za kupima kiwango cha taka ndogondogo kwenye maji ili wanafunzi na wananchi waelewe madhara ya taka za plastiki.

Mjini Mombasa hatua kubwa iliyofikiwa ni kufungwa kwa dampo la taka la Kibarani. Dampo hilo lilikuwa linachuruzisha taka zake za maji moja kwa moja baharini.

Goddfrey Nato  ambaye ni Waziri wa Mazingira kwenye Kaunti ya Mombasa alieleza kuwa “kuendelea kutumia eneo hilo la kutupa taka kulikuwa ni hatari kubwa kwa bayonuai ya bahari. Haikuwezekana tena kuendelea kulitumia kwa usalama wa mazingira.”

Hivi sasa taka zitatupwa kwenye eneo rafiki zaidi kwa mazingira.

Halikadhalika kukawepo na ahadi kutoka kampuni na taasisi 29 zikiwemo hoteli 17 zilizopo ufukweni Mombasa kupiga marufuku matumizi ya chupa na mirija ya plastiki na hoteli hizo ni pamoja na Tamarind na kundi la hoteli za Serena Inn .

UNEP nayo ilikuwepo Mombasa ambapo afisa wake kutoka ofisi ya Afrika, Cyrille-Lazare Siewe alisema wakati wa tukio hilo kuwa “kwa kuleta pamoja sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau wote, hili ni jukumu la UN Environment sasa na tunatumai watu wengi zaidi wataungana nasi,na tunatumai nchi zote pia kote duniani zitachukua hatua na kusema tunataka kuleta mabadiliko, tunataka kupambana na uchafuzi wa mazingira.”

Safari ya kilometa 35 kutoka Mombasa hadi Diani ilitamatishwa na shamrashamra nyingi ikizingatiwa kuwa ni nyumbani kwa Dipesh, kiongozi wa mradi wa Flipflopi.

Msanii mashuhuri nchini Kenya Muthoni Ndonga ambaye ni balozi mwema wa mradi wa Flipflopi aliyeahidi kutumia kipaji chake kusaidia na kuchochea mapinduzi katika matumizi ya plastiki kwa kusambaza ujumbe ya kwamba matumizi ya mara moja tu ya plastiki hayana maana yoyote.

Akizungumza kwenye shamrashamra za kupokea dau hilo mjini Diani, Muthoni amesema, “tunaanza kubadili mazungumzo..tunapaswa kufikiria jinsi ya kutunga sheria na kuzisimamia kuhusu matumizi ya mara moja ya plastiki —lakini wakati huo huo kwa kuwa tayari tunazo plastiki lazima tufikirie jinsi gani tunaweza kuzitumia tena na tena kwa matumizi bora.”

Mabaharia wa Flipflopi wakiongozwa na nahonda Skanda wameonyesha matumaini makubwa kwani wao binafsi kupitia safari yao wameweza kuzungumza moja kwa moja na wananchi wapatao 1,000 na kuwajulisha umuhimu wa fikra mbadala katika kuondokana na taka za plastiki.

Dau la kijadi lenye urefu wa mita 9 lilolotengenezwa kwa tani  10 za mabaki ya plastiki, litakuwa dau la kwanza la aina yake kuzinduliwa na kuanza safari yake tarehe 24 mwezi huu wa Januari kutoka Lamu Kenya mpaka Zanzibar Tanzania.
UN Environment
Dau la kijadi lenye urefu wa mita 9 lilolotengenezwa kwa tani 10 za mabaki ya plastiki, litakuwa dau la kwanza la aina yake kuzinduliwa na kuanza safari yake tarehe 24 mwezi huu wa Januari kutoka Lamu Kenya mpaka Zanzibar Tanzania.

Na baada ya safari ya kilometa 500 walitia nanga Mji Mkongwe wakati muafaka kabisa sambamba na tamasha la Sauti za Busara, ambalo hutumika kusherehekea tamaduni, ubunifu na maadili ya nchi za Afrika Mashariki.

 “Tumefurahi sana kukabirisha Zanzibar dau la FlipFlopi lililosafiri likipigia kampeni bahari safi. Safari yenyewe, na nia ya ubunifu ndani yake ni ishara ya kile ambacho kinaweza kufanyika kuleta mabadiliko,” amesema Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar.

Akatumia fursa hiyo kuahidi kwamba Zanzibar imeazimia kupiga vita uchafuzi utokanao na matumizi ya plastiki na “tutaendelea kushirikiana na wananchi wote kusaka majawabu ya changamoto za kimazingira zinazoendelea kuibuka.”

Naye Siim Kiisler, ambaye ni Waziri wa Mazingira wa Estonia na Rais wa mkutano wa Nne wa Baraza Kuu la shirika la mazingira duniani, UNEP, utakaofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 15 mwezi ujao mjini Nairobi, Kenya amesema huko Mji Mkongwe kuwa  “ni dhahiri kuwa kampeni ya Bahari Safi kupitia dau la Fliflopi inahamasisha wananchi kutoka Afrika na maeneo mbalimbali duniani kufahamu zaidi juu ya suala la dharura la kimazingira linalokabili dunia hivi sasa.”

“Kwa kufanya safari hii ya kishujaa, timu hii imethibitisha kile kinachowezekana pindi tunapotumia majawabu bunifu na kutatua kwa njia tofauti changamoto ya uchafuzi wa taka za plastiki,” amesema Bwana Kiisler.

Hitimisho la safari ya Flipflopi Mji Mkongwe huko Zanzibar ni mwanzo wa safari nyingine ya kurejea Nairobi, Kenya ambapo dau hilo litawekwa kwenye eneo la mkutano wa UNEA.

Wakati wa mkutano huo unaoleta viongozi wa ngazi ya juu kabisa wakiwemo marais na wabobezi wa mazingira, dau hilo litatumika kudhihirisha kile kinachoweza kufanyika kutatua changamoto ya plastiki pindi ubunifu na fikra mbadala zinapotumika.

Kampeni ya #CleanSeas ilianzishwa na UNEP mwezi Februari mwaka 2017 ikilenga kushirikisha serikali, jamii, asasi za kiraia na sekta binafsi juu ya harakati za kutokomeza uchafuzi wa bahari.

Kampeni hiyo inalenga kubadili tabia, viwango na sera duniani kote ili kupunguza uchafuzi wa bahari.