DRC ni kimbilio kwa maelfu ya watu wanaokimbia machafuko Sudan Kusini
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema limeshuhudia ongezeko la wakimbizi kutoka nchini Sudan Kusini wanaowasili nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,DRC.
Akizungumza na waandishi habari mjini Geneva, Uswisi hii leo msemaji wa UNHCR Babar Baloch amesema maelfu ya watu walio na wasiwasi wa usalama wao wamevuka mpaka kufuatia mapigano yanayolenga raia.
“Inakadiriwa kuwa wakimbizi 5000 wamewasili katika vijiji vya mpakani karibu na mji wa Ingbokolo, kaskazini mashariki mwa jimbo la Ituri kwa mujibu wa machifu walioko mashinani. Kuna ripoti kuwa watu wengine 8,000 wamefurushwa makwao, vitongoji vya mji wa Yei.”
Kwa mujibu wa UNHCR, watu wanakimbia mapigano yaliyozuka Januari 19 mwaka huu kati ya jeshi la serikali na kundi lililojihami la National Salvation Front katika jimbo la Equatoria kati linalopakana na DRC na Uganda.
“Nchini DRC wale wanaokimbia machafuko Sudan Kusini waliwasili kwa miguu mwishoni mwa wiki, wengi ni wanawake, watoto na wazee. Waliwasili wakiwa wamechoka, wana njaa na kiu. Miongoni mwao kuna wanaoumwa malaria na magonjwa mengine.”
UNHCR imeongeza kuwa idadi kubwa ya wanaowasili wamekumbwa na kiwewe baada ya kushihidia ukatili ikiwemo watu waliojihami wakiua, kubaka na kupora vijiji.