Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhuru wa mahakama uko hatarini Nigeria yaonya UN

Mtaalam maalumu wa Umoja wa mataifa kuhusu uhuru wa mahakama na mawakili, Diego Garcia-Sayán
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Mtaalam maalumu wa Umoja wa mataifa kuhusu uhuru wa mahakama na mawakili, Diego Garcia-Sayán

Uhuru wa mahakama uko hatarini Nigeria yaonya UN

Haki za binadamu

Mtaalam maalumu wa Umoja wa mataifa kuhusu uhuru wa mahakama na mawakili, Diego Garcia-Sayán, leo ameonya kwamba hatua ya Rais wa Nigeria kumsitisha kazi na kumbadilisha mwanasheria mkuu wan chi hiyo ni kinyume na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu kuhusu uhuru wa mahakama na kutenganisha madaraka.

Bwana Garcia-Sayán amesema viwango hivyo vya haki za binadamu vya kimataifa vinabainisha kwamba majaji wanaweza kufutwa kazi tu endapo hawawezi kutekeleza majukumu yao au kwa misingi maalum, na uamuzi wowote wa kumsitisha au kumfukuza kazi jaji ni lazima uwe wa haki na uchukuliwe na mamlaka huru kama vile baraza la mahakama au mahakama.

Ameongeza kuwa kitendo cha kuwafukuza majaji bila kufuata utaratibu unaostahili kisheria na bila kuwepo kwa ulinzi muafaka wa mahakama wa kupinga uamuzi huo ni kwenda kinyume na misingi ya uhuru wa mahakama.

Mwanasheria huyo mkuu Walter Onnoghen alisimamishwa kazi tarehe 25 Januari 2019 na nafasi yake kupewa Ibrahim Tanko Mohammad. Rais wa Nigeria kwa upande wake amesema amechukua hatua hiyo kwa kuzingatia amri iliyotolewa siku mbili kabla na mahakama iliyoanzishwa kwa misingi ya katiba kwa madai ya kukiuka maadili ya kazi.

Hata hivyo mahakama nne tofauti nchini Nigeria ikiwemo mahakama ya rufaa na mahakama mbili kuu  zote zilitoa uamuzi wa kutaka mwanasheria huyo aendelee kubaki.

Mtaatamu wa Umoja wa Mataifa ameikumbusha Nigeria kwamba taasisi zote za serikali zinapaswa kuzingatia maamuzi ya mahakama za kitaifa na mahakama kuu.

Nigeria hivi sasa iko katika maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwishoni mwa wiki hii.