Mchango wa wanawake na wasichana katika sayansi ni muhimu sana:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihudhuria mkutano ulioandaliwa na UN Women kuhusu sayansi,teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) kuhusu programu za kompyuta.
UN Photo/Antonio Fiorente
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihudhuria mkutano ulioandaliwa na UN Women kuhusu sayansi,teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) kuhusu programu za kompyuta.

Mchango wa wanawake na wasichana katika sayansi ni muhimu sana:Guterres

Wanawake

Ujuzi katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati unachagiza ubunifu na ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika sayansi.

Guterres katika ujumbe wa wa siku hii ambayo huadhimishwa kila mwaka Februari 11 amesema, wanawake na wasichana ni wa muhimu katika maeneo yote haya, lakini bado uwakilishi wao ni mdogo na kuongeza kuwa ,“misimamo ya kijinsia, ukosefu wa watu ambao ni mifano inayoonekana na sera na mazingira yasiyofaa au hata ya uadui vinaweza kuwazuia kuingia katika kazi hizi.”

Amesisitiza kwamba dunia haiwezi kumudu kukosa mchango wa nusu ya watu wote duniani, hivyo juhudi za pamoja  zinahitajika ili kukabiliana na vikwazo hivi ikiwa ni pamoja na hisia zisizofaa kuhusu uwezo wa wasichana. Na kwamba ni lazima ,“tuchagize fursa za kupata elimu kwa wanawake na wasichana , hususan maeneo ya vijijini.”

Katibu Mkuu amehimiza juhudi zaidi za kubadili utamaduni wa mahali pa kazi ili wasichana ambao wanapenda kuwa wanasayansi, wahandisi na wataalamu wa hisabati waweze kufurahia na kutimiza ndoto  zao za kazi katika nyanja hizi.

Ametoa wito wa  kuhakikisha kwamba kila msichana, kila mahali ana fursa ya kutimiza ndoto zake, kukuza uwezo wake na kuchangia katika mustakabali  endelevu kwa wote.