Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatimaye katiba ya Myanmar kufanyiwa marekebisho, UN yapongeza

Mjumbe maalum wa haki za binadamu kuhusu Myanmar Yanghee Lee
Picha/Jean-Marc Ferré
Mjumbe maalum wa haki za binadamu kuhusu Myanmar Yanghee Lee

Hatimaye katiba ya Myanmar kufanyiwa marekebisho, UN yapongeza

Haki za binadamu

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Myanmar, Yang Lee amekaribisha hatua ya kuanzishwa kwa kamati ya bunge itakayoshughulikia marekebisho ya katiba nchini humo.

Bi. Lee ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Myanmar hususan kwenye vipengele vya katiba vinavyonyima haki za msingi wananchi wakiwemo waislamu wa kabila la Rohingya, amesema, “kuanzishwa kwa kamati hiyo ni maendeleo chanya na natumaini itasaidia Myanmar kuwa na mpito dhahiri wa kidemokrasia.”

Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi, imesema mtaalamu huyo amesisitiza kuwa wananchi wanatamani katiba ifanyiwe marekebisho na amesihi kamati hiyo mpya ya pamoja itekeleze matakwa ya wananchi.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mwka 2015, chama tawala cha National League for Democracy, NDL, kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi, kiliahidi marekebisho ya katiba na kilishinda uchaguzi huo kwa kishindo.

Katiba ya Myanmar yam waka 2008 iliandaliwa na serikali iliyopita ya kijeshi na kwa muda mrefu imekuwa kikwazo kikubwa cha kusongesha mabadiliko kutoka utawala wa kijeshi kwenda wa kidemokrasia.

Mathalani katiba hiyo inatenga asilimia 25 ya viti vya bunge kwa wanajeshi na pia inapatia jeshi mamlaka ya kudhibiti wizara ya mambo ya ndani, ulinzi na mipaka.

“Katiba ya sasa si ya kidemokrasia,” amesema Bi. Yang Lee na kwamba Myanmar haiwezi kutambuliwa kuwa ni nchi ya kidemokrasia hadi pale katiba hiyo inafanyiwa marekebisho.