Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 15 za mfuko wa ‘Elimu haiwezi kusubiri’ zaanza kuleta manufaa kwa wakimbizi wa Sudan Kusini walioko Ethiopia.

Mkimbizi kutoka Sudan Kusini akifundisha katika shule ya Msingi kwenye kambi ya wakimbizi iitwayo Kule, nchini Ethiopia.
UNHCR/Petterik Wiggers
Mkimbizi kutoka Sudan Kusini akifundisha katika shule ya Msingi kwenye kambi ya wakimbizi iitwayo Kule, nchini Ethiopia.

Dola milioni 15 za mfuko wa ‘Elimu haiwezi kusubiri’ zaanza kuleta manufaa kwa wakimbizi wa Sudan Kusini walioko Ethiopia.

Utamaduni na Elimu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Ethiopia linasimamia uwekezaji wa mfuko wa dunia wa dola milioni 15 wa  kufanikisha mpango uliopewa jina ‘Elimu haiwezi kusubiri’wenye lengo la kuinua ubora wa elimu kwa wakimbizi na wenyej nchini humo. 

Uwekezaji wa ‘Elimu haiwezi kusubiri’ unajumuisha ujenzi wa shule tatu za mfano, madarasa 41 katika shule 8 za sekondari, madarasa 84 katika shule 4 za msingi na vifaa kama madawati, viti na chaki katiuka maeneo ya Benishangul-Gumuz na Gambella nchini Ethiopia, ambayo zaidi yanawapokea wakimbizi kutoka Sudan Kusini. 

Na Kama walivyo watoto wengi katika kambi ya wakimbizi ya Tierkidi iliyoko Gambella Ethiopia, Pal Biel Jany miaka mitano iliyopita alikimbia vurugu nchini mwake Sudan Kusini. Pal ana umri wa miaka 15 na katika siku za usoni ana ndoto ya kuwa rais wa Sudan Kusini.

Makala ya UNICEF Ethiopia inaonyesha wazazi wa mwanafunzi Pal wakiwa na imani kuwa kijana wao atapata elimu nzuri ili siku moja naye aweze kuwasaidia wadogo zake. 

Ni kwa mantiki hiyo,  familia yake imekubali aendelee kuishi na shangazi yake katika kambi ya Tierkidi kwa kuwa hakuna fursa za elimu nchini Sudan Kusini ambako wazazi wake wanaishi.

Pal ana bahati ya kuwa na Changkuoth Tel Wal kama mwalimu wake wa darasa la nne katika shule ya msingi Teirkidi. Mwalimu Changkuoth hakuwa amepewa fursa ya kupitia katika mfumo wa kawaida wa mafunzo ya ualimu lakini hali ilibadilika msimu wa kiangazi uliopita wakati yeye pamoja na wakimbizi wengine 343 waliambiwa wataweza kuingia chuoni na kupata stashahada ya ualimu. Sasa wanaweza kuwa walimu kamili na kuinua masomo kwa watoto wakimbizi.

Changkuoth anasema, “inaweza kuonekana namna ambavyo elimu ni nzuri kwa jamii na watoto. Sudan Kusini na hapa kambini kuna watu wengi wasio na elimu kuliko walionayo.”

Changkuoth Ter mwenye umri wa miaka 26, ni mwalimu wa masomo ya sayansi katika darasa la nne. Mkewe mwenye umri wa miaka 22 yuko darasa la 10 na anasoma katika shule ya sekondari iliyoko katika kambi hiyo hiyo ya wakimbizi. Binti yao mwenye umri wa miaka 6 anasoma katika shule hiyo hiyo ya Tierkidi namba 3.