Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lilikuwa suala la kifo na maisha. Kwa nini walikuwa wananinyima kibali cha kutibiwa?

Hospitali ya Ash Shifa mjini Gaza
OCHA
Hospitali ya Ash Shifa mjini Gaza

Lilikuwa suala la kifo na maisha. Kwa nini walikuwa wananinyima kibali cha kutibiwa?

Haki za binadamu

Baada ya kugundulika kuwa wanaugua saratani, wagonjwa kwenye eneo la Palestina la Gaza linalokaliwa na Israeli, hulazimika kusubiri kwa miezi kadhaa  kabla ya kupata matibabu. 

Hiyo ni kwa mujibu wa makala iliyochapishwa na shirika la afya duniani, WHO, kanda ya Mashariki ya Kati ikisema kuwa suala la kupatiwa kibali cha kwenda kutibiwa nje ya ukanda wa Gaza linaweza kuwa jambo gumu na ni mchakato usiotabirika na wengi wanaomba mara kadhaa kabla ya kupata nafasi ya kutoka nje. 

WHO inasema wengine wasio na bahati, hukosa kabisa kibali cha kutoka kwenda kupata matibabu wanayoyahitaji ilhali uwezo wa hospitali za Gaza kufanya uchunguzi wa kina na matibabu kwa wagonjwa wa saratani ni mdogo kutokana na uhaba wa dawa na vifaa tiba.

"Wagonjwa wengi wanahitaji huduma ya afya mahali kwingine katika jimbo lililokaliwa la Palestina au katika nchi za nje lakini kuondoka Gaza, wagonjwa wanalazimika kupata kibali kwa mamlaka za Israel. Mwaka 2018 asilimia 39 ya wagonjwa walioomba vibali vya kuondoka Gaza kwa ajili ya matibabu hawakupata ruhusa za kuondoka." imesema makala hiyo kwenye wavuti wa WHO.

Miongoni mwa wagonjwa ni Samira mwenye umri wa miaka 64 ambaye aligundulika na saratani ya mfuko wa kizazi mwaka 2016. 

Samira alifanyiwa upasuaji kisha yakahitajika matibabu baada ya hapo ambayo hayapatikani Gaza na madaktari wakamwandikia akafanyiwe vipimo zaidi huko Yerusalem Mashariki.

WHO inasema ilimchukua Samira zaidi ya miezi 6 na maombi ya kibali mara tano mpaka aliporuhusiwa mwaka 2018 ambapo Samira anasema,  “wakati wote huu nilikuwa navuja damu zisizo za kawaida. Ilikuwa suala la maisha na kifo. Kwa nini nilikuwa nanyimwa kibali?”

Kwa kutambua kuwa matibabu ni haki ya msingi ya kila mtu, shirika la afya duniani linatoa wito kulinda na kutimiza haki ya afya kwa wapalestina wote.