Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhasama wa kibiashara kati ya Marekani na China haunufaishi upande wowote- UNCTAD

Shehena za usafirishaji mizigo kwenye bandari katika Jamhuri ya Kidmokrasia ya São Tomé na Príncipe
UNCTAD/Jan Hoffmann
Shehena za usafirishaji mizigo kwenye bandari katika Jamhuri ya Kidmokrasia ya São Tomé na Príncipe

Uhasama wa kibiashara kati ya Marekani na China haunufaishi upande wowote- UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Uhasama wa kibiashara wa nipe nikupe kati ya China na Marekani huenda usiwalinde wazalishaji wa ndani wa nchi hizo mbili na unaweza kuwa na madhara makubwa kwa uchumi duniani iwapo hautadhibitiwa, imesema Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD  hii leo.

Kwa mujibu wa ripoti ya kamati hiyo, mauzo ya dola bilioni 250 ya bidhaa zinaouzwa na China nje ya nchi hiyo ambazo zinapaswa kulipiwa ushuru nchini Marekani, ni asilimia sita tu ya bidhaa hizo zitanunuliwa na kampuni za Marekani.

Aidha utafiti unaonyesha mauzo ya takriban dola bilioni 85 ya bidhaa kutoka  Marekani ni asilimia 5 tu ya zile zinazohitaji kutozwa ushuru nchini China ndio zitanunuliwa na kampuni za China.

Biashara ya mashine na kemikali iko hatarini

Kwa mujbu wa utafiti wa UNCTAD, madhara ni yale yale katika sekta mbalimbali ikiwemo kwenye sekta za mashine, samani, kemikali na vifaa vyavipimo huku ikiongeza kuwa ushuru unaotozwa na pande mbili utakuwa na athari ndogo kwa kampuni katika soko husika.

UNCTAD inasema kuwa iwapo Marekani na China hawataondoa mzozo wa kiushuru kufikia tarehe Mosi mwezi ujao wa Machi, ushuru kwa bidhaa za nchi moja kwa nyingine utaongezeka kwa asilimia 10 ya sasa hadi asilimia  25.

Ushuru ni sawa na mtu aliyejigeuzia bunduki

Akizindua ripoti hiyo mkurugenzi wa kitengo cha biashara ya kimataifa ya bidhaa na huduma, Pamela Coke-Hamilton amemnukuu aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Cordell Hull, akisema ushuru wa kujilinda ni kama, “bunduki inayojigeuza na kumlenga anayeishikilia,” ambayo ilisababisha kuanguka kwa uchumi miaka ya 1930.

Bi Hamilton amesema iwapo hali hiyo itasailia basi itakuwa na athari kubwa ambazo zitaathiri vibaya mwenendo wa kiuchumi kwa sababu za msukosuko katika soko la bidhaa na fedha.

Ameongeza kuwa kutakuwa na msukumo mkubwa wa ukuaji kiwamataifa, huku kampuni zikilizamika kuongeza bei itokanayo na mabadiliko ambayo yataathiri uwekezaji wa uzalishaji na faida.

 Washindi na watakaoathirika na uhasama wa kibiashara

Ripoti inasema mataifa ambayo yanatarajiwa kunufaika kutokana na uhasama wa kibiashara ni wanachama wa Muungano wa Ulaya ambapo huenda mauzo ya nje yataimarika kwa dola bilioni 70 huku Japan na Canada zikishuhudia mauzo ya nje kwa zaidi ya dola bilioni 20 kwa kila moja.

Licha ya kwamba takwimu hizo haziashirii kwa kiasi kikubwa mtizamo wa biashara kimataifa ambayo ni dola trilioni 17 kwa mwaka 2017- kwa baadhi ya nchi, kama Mexico, ongezeko la mauzo ya nje yatachangia asilimia 6 ya ongezeko ya mauzo nje kwa jumla.

Nchi zingine ambazo huenda zikanufaika na uhasama huu wa kibiashara ambao uliibuka mwaka 2018 ni pamoja na Australia na ongezeko la asilimia 4.6 ua mauzo ya nje, Brazil na 3.8, India 3.5, Ufilipino 3.2 na Vietnam na asilimia 5.

 Mauzo ya nje huenda yakapungua Asia Mashariki

Ripoti hiyo ya UNCTAD inaonya kuwa uhasam huo huenda ukapunguza mauzo ya nje kwa kiasi cha dola bilioni 160 katika ukanda huo iwapo hautatatuliwa kabla ya ukomo wake wa Machi.

Halikadhalika utafiti umeonyesha wasiwasi wa pamoja kuwa uhasama ho wa kibiashara huenda ukawa na atahri zisizozuilika kwa chumi za dunia ambazo ni dhaifu hususan ambazo zinakuwa, au zinazotegemea mauzo ya bidhaa nje

Kwa mujibu wa ripoti, moja ya wasiwasi ni kuwa uhasama wa kibiashara huenda ukawa vita vya kifedha na kufanya madeni yaliyokopeshwa kwa dola kuwa magumu zaidi kulipika.