UM hauegemei kundi lolote katika sakata la Venezuela:Guterres

4 Februari 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amesema kuhusu hali ya Venezuela kuna hatua kadhaa zilizoanzishwa na makundi mbalimbali katika kusaka suluhu ya mgogoro unaoendelea nchini humo.

Akiongeza kuwa Umoja wa Mataifa umewasiliana na makundi hayo lakini hautofungama na kundi lolote

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)

“Umoja wa Mataifa umeamua kutokuwa sehemu yoyote ya makundi haya ili kuendelea kutoa uaminifu wa kazi za ofisi yetu kwa pande zote husika na kuweza kwa ombi lao kusaidia kusaka suluhu ya kisiasa.”

Bwana Guaidó ambaye ni kiongozi wa upinzani, tarehe 23 mwezi Januari alijitangaza kuwa rais wa muda wa Venezuela, ilhali Rais Maduros aliapishwa rasmi kuendelea na wadhifa wa urais kufuatia uchaguzi uliofanyika nchini humo mwezi Mei mwaka jana.

Tayari Marekani na mataifa mengine ya Amerika ya Kusini yametangaza kumtambua Bwana Guaidó, huuku Muungano wa Ulaya ukitaka Rais Maduros aitishe upya uchaguzi huru na wa haki la sivyo nao watachukua hatua kwa mujibu wa kipengele namba 233 cha katiba ya Venezuela kinachotambua uwepo wa Kaimu Rais.

Hata hivyo Urusi na mataifa mengine kama vile Afrika Kusini na Equatorial Guinea zimesema suala la Venezuela ni suala la ndani ya nchi hiyo na halipaswi kuingiliwa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud