Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mke wangu ni shujaa- Samir Al Sayed, mkimbizi kutoka Syria

Wakimbizi wa Syria wakiwa mbioni kutafuta makazi
UNICEF/UN0277723/Souleiman
Wakimbizi wa Syria wakiwa mbioni kutafuta makazi

Mke wangu ni shujaa- Samir Al Sayed, mkimbizi kutoka Syria

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakimbizi wawili wa Syria Wafika na Taha wameishi muda mrefu wa maisha yao wakiwa ndani, wakihangaika kusogea, kuwasiliana na kuchangamana na watu walio karibu yao. Wazazi wao wakikabiliana na uhaba wa huduma kwa ajili ya watu wenye ulemavu, sasa wanaomba msaada wa kupatiwa makazi katika nchi nyingine duniani ambako watawapa huduma nzuri watoto wao. 

Wakiwa wamezaliwa na tatizo la mtindio wa ubongo, hali ambayo inaathiri uwezo wao wa kuona, kuzungumza, kusikia na kutembea, Wafika mwenye umri wa miaka 35 na Taha wa umri wa miaka 25, wanahitaji huduma maalumu ya matibabu na uangalizi wa kijamii. Asili ya familia hii ni Damascus ambako walikimbia vita nchini Syria mwaka 2013 na kutafuta makazi Misri.

Mama yao, Bi Maysa anawahudumia kwa kila mahitaji yao. Anasema kila asubuhi anambadilisha nguo Wafika ambaye ni wa kike na kumwogesha. NayeTaha wa kiume anamtaka mama yake tu.

(Sauti ya Maysaa Al Sayed)

 “Ninamnyoa ndevu, ninamwogesha na kumbadilisha nguo. Hawezi kumruhusu mtu mwingine kumwogesha. Ananiruhusu mimi tu kumlisha”

Maysaa anasema angependa kuwapatia watoto wake fursa nzuri, huduma nzuri na matibabu mazuri.

Baba yao, Mzee Samir Al Sayed alipata matatizo ya mgongo kwa sababu ya kuwabeba watoto wake. Anasema angependa kumpunguzia mzigo mke wake.

(Sauti ya Samir Al Sayed)

 “Ninamheshimu sana mke wangu. Anachokifanya ni kitendo cha kishujaa”

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linatekeleza mpango wa kuwahamisha wakimbizi katika zaidi ya nchi 65 duniani kote na linakadiria kuwa wakimbizi milioni 1.4 watahitaji kutafutiwa makazi katika nchi nyingine kwa mwaka huu wa 2019 likiwa ni ongezeko la asilimia 17 tangu mwaka uliopita wa 2018.