Raia 1000 wa Ghana wamerejea nyumbani kwa hiyari toka Libya na Niger tangu 2017-IOM

1 Februari 2019

Leo shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limesema litimiza na kuzidi lengo la kuwarejesha nyumbani kwa hiyari raia 650 wa Ghana waliokuwa nchini Libya na Niger.

Shirika hilo lililopewa jukumu mwaka 2016 kutekeleza mpango wa kuwarejesha nyumbani kwa hiyari wahamiaji na wakimbizi waliokwama Libya wakiwa mbioni kwenda Ulaya kusaka maisha bora, limesema kwa Ghana katika kipindi cha miaka mitatu lilipaswa kuwarudisha nyumbani raia wan chi hiyo 650, lakini hadi kufikia mwisho wa Januari mwaka huu IOM imefanikiwa kuwarejesha Ghana jumla ya raia 1001, hatua ambayo imetimiza lengo na zaidi.

Kwa mujibu wa IOM mradi huo utaendelea hadi mwaka 2020 na ndege ya karibuni kabisa ikiwa na wahamiaji hao iliwasili Ghana 25 Januari. Raia wa nchi hiyo waliorejea kwa hiyari wamelishukuru shirika la IOM kwa kuwasaidia kufufua matumaini yao ya maisha miongoni mwao ni Fusseini “Ninafurahi kwamba nimerejea nyumbani kwa familia yangu. Sikupoteza maisha nikiwa safarini au nikiwa Libya. Hatimaye nimerejea nyumbani.” Fausseini ni miongoni mwa raia wa Ghana walioshiriki safari ya kwanza kabisa ya mradi wa IOM wa kurejea nyumbani kwa hiyari mwaka 2017. Hivi sasa anatarajia kufungua duka la nguo kuendesha maisha yake.

Mradi huo wa IOM unapigwa jeki na Muungano wa Ulaya na lengo ni kuwapa fursa mpya wahamiaji hao wanaochukua safari za hatari kurejea nyumbani na kuendesha maisha. Shirika hilo linawapa watu wote wanaorejea msaada wa kuanzia ikiwemo fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya lazima. Pia wanapatiwa msaada wa matibabu, ushauri nasaha na mafunzo ya vitendo yatakayowawezesha kujitegemea.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter