Sisi tukisameheana, watu watatoka kote duniani na kusema alaa! kumbe Sudan Kusini ni pahala pazuri

1 Februari 2019

Mapema wiki hii mjini Juba Sudan Kusini imefanyika mechi ya mpira wa miguu kwa ajili ya kuhamasisha amani kwa kuwaleta watu pamoja. Chini ya jua kali timu A na B za vijana wa umri wa chini ya miaka 23 zilikwaana katika ushindani mkali kwa lengo la kusambaza ujumbe wa amani na umoja kwa mamia ya mashabiki waliohudhuria.

Kijana Chika Sydney Edward Joshua amecheza mpira wa miguu kwa miaka 6 pekee na tayari amefika ngazi ya taifa. Ana matumaini kuwa mapigano yataisha ili aweze kupata nafasi ya kuwa mchjezaji wa kulipwa katika soka, anayoiita “mchezo mzuri unaounganisha watu”

(Sauti ya Chika Sydney Edward Joshua)

“Huu ni wakati wa watu wa Sudan Kusini kusameheana. Tunapaswa kusameheana. Sisi ni taifa moja, ni watu wamoja. Tusahau yaliyopita na tugange yajayo. Ninapoiangalia nchi yetu kuna matuaini ya siku za usoni kama tutasameheana na nchi hii itakua zaidi na kuwa sehemu nzuri kwa kila mtu kuja kutoka kila pembe ya Dunia. Watakuja hapa na kufurahi, kila wakati wakirejea makwao watatasema, wow, Sudan Kusini ni eneo zuri”

Pamoja na viongozi mbalimbali waliokuwepo akiwemo Makamu wa Rais wa Sudan Kusini James Wani Igga, Mwanamuziki mkongwe wa Sudan Kusini Emmanuel Kembe aliwanyanyua watu kwenye viti kwa midundo yake

Watu wana matumaini na makubaliano yaliyotiwa saini mwaka jana. Wana matumaini kuwa hatima ya kudumu ya vurugu itahamasisha uwekezaji katika maendeleo na kuwapa vijana wa Sudan Kusini nafasi ya kufikia mafanikio.

Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini pamoja na jumuiya ya kimataifa wanaunga mkono juhudi za kuleta amani nchini kote inagawa bado wasiwasi upo kutokana na kuzorota kwa utekelezaji wa mkataba.  Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan kusini na mkuu wa UNMISS David Shearer anasema, 

(Sauti ya David Shearer)

"Ninafikiri kuna matumaini kwa watu na ni jukumu letu kwa pamoja kuhakikisha tunaendelea kuyajenga hayo matumaini na kuhakikisha yanaendelea”

Tumaini kubwa ni kuwa kukiwa na amani ya kudumu, fursa na mafanikio zitakuja kwa watu wote hususani kwa kizazi kijacho na viongozi wa baadaye wa Sudan Kusini.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter