Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ibrahim Thiaw wa Mauritania ateuliwa kuongoza vita dhidi ya hali ya jangwa

Ibrahim Thiaw, Mshauri maalum wa UN kuhusu Sahel .
UN News/Daniel Dickinson
Ibrahim Thiaw, Mshauri maalum wa UN kuhusu Sahel .

Ibrahim Thiaw wa Mauritania ateuliwa kuongoza vita dhidi ya hali ya jangwa

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, leo amemteua Ibrahim Thiaw kutoka Mauritania kuwa Katibu Mkuu mtendaji mpya wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na hali ya jangwa (UNCCD).

Uteuzi huo umefuatia mahsuriano na ofisi ya UNCCD , na bwana Thiaw atachukua nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Bi. Monique Barbut wa Ufaransa, ambaye Katibu Mkuu amemshukuru kwa uwajibikaji wake na kujitoa kuhudumia Umoja wa Mataifa.

Bwana. Thiaw anachukua wadhifa huo akiwa na uzoefu wa takriban miaka 40 katika masuala ya maendeleo endelevu, utawala wa mazingira na udhibiti wa maliasili. Hivi karibuni amekuwa mshauri maalumu wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya Sahel.

Kabla ya uteuzi huu alishinka nyadhifa mbalimbali kwenye Umoja wa Mataifa ikiwemo naibu mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira (UNEP) tangu 2013-2018 ambako alifanya kazi kubwa ikiwemo kuundwa kwa Baraza Kuu la Mazingira la Umoja wa Mataifa.

Thiaw alijiunga na Umoja wa Mataifa mwaka 2007 kama mkurugenzi wa kitengo cha utekelezaji wa sera za mazingira cha UNEP. Kabla ya kujiunga na Umoja wa Mataifa alifanya kazi na muungano wa kimataifa wa hifadhi ya maliasili (IUCN) kama mkurugenzi wa kanda ya Afrika Magharibi na baadaye kama kaimu mkurugenzi mkuu.

Lakini ujuzi wa Bwana. Thiaw ulianzia nyumbani nchini mwake Mauritania ambako alihudumu kwa miaka 10 katika wizara ya maendeleo vijijini. Ana stashahada ya uzamili katika masuala ya misitu na mbinu za uzalishaji wa bidhaa za misitu.