Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziarani Somalia, Di Carlo awahakikishia viongozi ushirikiano wa UN

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kisiasa akiwa ziarani nchini Somalia alipokutana na Rais wa shirikisho la Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed Farmajo mwezi juni 2018
Picha ya UM/Omar Abdisalan
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kisiasa akiwa ziarani nchini Somalia alipokutana na Rais wa shirikisho la Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed Farmajo mwezi juni 2018

Ziarani Somalia, Di Carlo awahakikishia viongozi ushirikiano wa UN

Masuala ya UM

Mkuu wa Idara ya Siasa kwenye Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo amewasili nchini Somalia leo ambapo amekaribishwa na  rais Mohamed Abdullahi Mohamed na Waziri Mkuu Hassan Ali Khaire, imesema taarifa ya pamoja iliyochapishwa kwenye wavuti wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bi. Dicarlo amefanya majadiliano na viongozi hao na kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Shirikisho la Somalia  na Umoja wa Mataifa.

Watatu hao wamejadili hatua ya serikali ya shirikisho ya Somalia na Umoja wa Mataifa kufanya kazi kwa karibu zaidi kwa manufaa ya watu wote wa Somalia na kuunga mkono ujenzi wa serikali ya Somalia na uendelezaji wa mchakato wa amani.

Bi. Dicarlo katika mazungumzo yake na mawaziri wa serikali ya shirikisho amesema kuna umuhimu katika uboreshaji wa uwiano katika ya wizara hiyo na Umoja wa Mataifa.

Aidha amepongeza ajenda ya mageuzi ya serikali ya Somalia na kuelezea utayari wa Umoja wa Mataifa kusaidia  katika utekelezaji wa mambo muhimu yaliyowekwa na serikali ikiwemo, siasa jumuishi, usalama na haki, uimarishaji uchumi, na maendeleo ya kijamii.

Waziri Mkuu, kwa upande wake, amesifu kazi za Umoja wa Mataifa Somali ikiwa ni miongoni mwa wanachama wa umoja huo na kusisitiza ahadi ya Somalia kwa majukumu yake ya kimataifa kama mwanachama. Waziri Mkuu pia ameshukuru jukumu muhimu la Umoja wa Mataifa nchini Somalia na mchango wake katika kusaidia Somalia kwenye safari ya kuondokana na migogoro na kuelekea utulivu , amani na ukuaji.

Viongozi  hao wa Somalia wameonyesha mshikamano na ushirikiano na Umoja wa Mataifa baada ya shambulio la kiwanja cha Umoja wa Mataifa mnamo Januari mosi mwaka huu wa 2019. Wamesisitiza ahadi yao ya kuhakikisha amani na usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

Serikali ya Shirikisho la Somalia na Umoja wa Mataifa wanatarajia kuimarisha ushirikiano wao wa muda mrefu ili kuiwezesha Somalia kuendelea kufanya maendeleo ya baadaye ya amani na mustakabali bora.