Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukwaa lazinduliwa kuhakikisha  teknolojia za kisasa za tiba zinafikia maskini

Watoto wakiwa na vidonge vyao tayari kumeza ili kujikinga dhidi ya magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, NTDs
WHO
Watoto wakiwa na vidonge vyao tayari kumeza ili kujikinga dhidi ya magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, NTDs

Jukwaa lazinduliwa kuhakikisha  teknolojia za kisasa za tiba zinafikia maskini

Afya

Wadau wa afya duniani kwa kutambua udharura wa kutengeneza tiba mpya za kuokoa maisha dhidi ya magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, NTDs, Malaria na Kifua Kikuu, leo wamezindua jukwaa la majadiliano ili kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwenye maeneo ambako bado ni tatizo kubwa.

Taarifa ya UNDP iliyotolewa leo  huko Bangkok, Thailand imesema jukwaa hilo linajumuisha wadau kadhaa ikiwemo serikali ya Japan, udau unaoongozwa na UNDP katika upatikanaji wa huduma za afya, ADP, linaunganisha nguvu ili kuboresha ubunifu wa teknolojia, mbinu na upatikanaji wa dawa, chanzo na huduma za utambuzi wa magonjwa ili hatimaye kufanikisha lengo la afya kwa wote.

Wadau hao wamesema wakati dunia katika miaka ya hivi karibuni imepata maendeleo makubwa kwenye sekta ya afya, bado mamilioni ya watu hawapati teknolojia mpya za afya ambazo ni muhimu kwa wao kuchanua na kustawi.

“Magonjwa yanayokumba watu maskini zaidi duniani kama vile NTDs, mara nyingi yamekuwa hayapati ufadhili wa fedha zinazohitajika ili kubuni teknolojia za kuyatokomeza. Na hata pale tiba inapopatikana, mara nyingi haifikii walengwa,” imesema taarifa hiyo.

Japan ni moja ya wadau kwenye jukwaa hilo ambapo afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo Sumi Manabu amesema, “katu hatuwezi kufikia lengo la afya kwa wote duniani bila kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na teknolojia za kuboresha huduma hiyo. Serikali  ya Japan inaona ni heshima kubwa kusaidia mashauriano baina ya wadau wakuu juu ya suala hili muhimu kama hatua ya kwanza ya kuchagiza ushirikiano unaohitajika kufanikisha malengo hayo.”

Wadau wengine ni GHIT wanaohusika na ubunifu wa teknolojia za afya duniani ambapo afisa mtendaji wake mkuu BT Slingby amesema “sasa kuliko wakati wowote ule ni muhimu kuungainsha majadiliano yetu kuhusu afya duniani na utafiti kwa maendeleo na kuangazia upatikanaji na usambazaji wa huduma za afya.”

Amesema kwa kuleta pamoja wadau muhimu, tunatarajia kufanyia marekebisho makubwa uchangiaji wa fedha kwenye masuala uchangiaji fedha, ugunduzi, utengenezaji na usambazaji wa dawa na teknolojia nyingine za afya.