UN inashirikiana na serikali Tanzania kubaini chanzo cha mauaji ya watoto 10 mkoani Njombe

30 Januari 2019

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kufuatia mauaji ya watoto kumi katika mkoa wa kusini mwa Tanzania wa Njombe  ambako yaelezwa kuwa viungo vya mwili vya watoto hao vilinyofolewa.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Stella Vuzo wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam, mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa, nchini Tanzania,  Álvaro Rodríguez amesema, kwa mujibu wa taarifa walizopokea kati ya watoto hao kumi, watatu ni wa familia moja ambapo miili yao ilikuwa imenyofolewa viungo ikiwemo sehemu zao za siri na akaongeza“hatuna taarifa kamili, kwa sasa tumetoa  ujumbe kwa serikali tukielezea serikali kuhusu wasi wasi wetu kufuatia tukio hilo kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano kutoka kwa serikali kupitia mamlaka ya mkoa wa Njombe, kufuatilia na kufikisha watekelezaji mbele ya vyombo vya sheria na kuhakikisha ulinzi kwa watoto wanaokwenda na kurudi kutoka shuleni”.

Kuhusu sababu ambayo huenda imechochea mauaji hayo, bwana Rodríguez amesema kuna madai kuwa inatokana na imani za kishirikina na kuongezaKumekuwa na matukio ya mauji ya watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi lakini visa vya aina hiyo vimepungua kwa kiasi kikubwa na havijasikika katika kipindi cha takriban miaka mitatu, kwa hiyo tumeshtushwa sana na mauaji haya”.

Yaelezwa kuwa kufikia sasa kuna watu ambao wamekamatwa kwa madai ya kutekeleza uhalifu huo. Umoja wa Mataifa unashirikiana na mamlaka husika katika kufuatilia kesi hii na wakati huo huo bwana Rodriguez akielezea msisitizo wa dawati la jinsia na watoto kwa ajili ya kuimarisha taarifa kwa polisi kuhusu matukio mbali mbali.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter