Umoja wa Mataifa walaani mauaji ya watoto mkoani Njombe Tanzania.
Umoja wa Mataifa nchini Tanzania umeeleza kusikitishwa kwake na mauaji ya watoto yaliyotokea mkoani Njombe nchini humo.
Taarifa iliyochapishwa leo katika tovuti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Tanzania, imemnukuu mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Alvaro Rodriguez amesema, “mashambulizi dhidi ya watoto hayakubaliki. Watoto wana haki ya msingi ya kuwa salama na kulindwa dhidi ya vurugu ili waweze kufurahia utoto wao na kukua. Umoja wa Mataifa unaungana na serikali ya Tanzania kulaani matendo haya maovu. Tuko tayari kusaidiana na serikali katika kulishughulikia suala hili.”
Aidha bwana Rodriguez ametoa wito kwa wadau wote kuungana katika kuhakikisha kuwa nyumba, shule na jamii zinakuwa maeneo salama kwa watoto.
Naye mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Tanzania Bi Maniza Zaman amesema, “watoto wanawekwa katika mazingira ya vurugu na unyonyaji katika maeneo mengi ya dunia. Hili linapaswa kukoma. Hakuna aina yoyote ya vurugu au manyanyaso dhidi ya mtoto ambayo yanakubalika au kuruhusiwa kwa sababu yoyote ile na kwa hivyo tendo lolote la namna hiyo ni kukiuka haki zao za msingi”
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Tanzania watoto 10, watatu wakiwa wa familia moja wamekutwa wakiwa wamefariki katika mazingira ambayo bado yanawatatanisha wanajamii na vyombo vya usalama.