Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP na FIFA waungana kuimarisha masomo na michezo shuleni

Helikopta ya WFP ikisambaza chakula
UNICEF/Peter Martell
Helikopta ya WFP ikisambaza chakula

WFP na FIFA waungana kuimarisha masomo na michezo shuleni

Utamaduni na Elimu

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP na shirikisho la soka duniani, FIFA wamekubaliana kutumia mpango wa mpira shuleni unaondesha na FIFA na ule wa mlo shuleni unaondeshwa na WFP, kuimarisha stadi za wanafunzi kama njia mojawapo ya kujenga jamii imara, endelevu na zenye ustawi. 

Msemaji wa WFP mjini Geneva, Uswisi, Herve Verhossel, akizungumza na waandishi wa habari hii leo amesema  FIFA inatambua kuwa mpango wa soka shuleni unalenga kufanya mpira uchezwe na watoto wa kike na wa kiume kupitia somo la elimu ya viungo na kuchangia katika elimu ya mtoto.

Amefafanua kuwa mpango wa mlo wenye lishe shuleni kupitia WFP unasaidia watoto kushiriki vyema kwenye masomo pamoja na michezo.

Kwa mantiki hiyo amesema kwa kuzingatia uzoefu na mtandao wa mashirika hayo mawili katika  utekelezaji wa miradi hiyo,

(Sauti ya Herve Verhossel)

“Mpango huu utasambaza mipira milioni 11 kwenye shule zilizopo katika nchi 211 zenye vilabu vya soka wanachama wa FIFA na kufikia watoto milioni 700. Kupitia mpango huu utakaochochea watoto kujiandikisha na kusalia shuleni, mradi wa mlo shuleni unaandaa watoto kuwa na mustakabali bora na kuboresha afya, elimu na tija. Faida hizo kwa pamoja na ushawishi wa soka kama mchezo unaounganisha watu wengi, miradi ya mlo na michezo shuleni kwa pamoja inaweza kuwapatia mamilioni ya watoto fursa ya kufikia ndoto zao.”

Kwa mujibu wa Verhossel, mkuu wa WFP David Besley na Gianni Infantino wa FIFA walikutana huko Davos, Uswisi kando ya jukwaa la uchumi duniani na kukamilisha makubaliano hayo ambayo katika robo ya tatu ya mwaka huu, mashirika hayo mawili yataanza utekelezaji wa mradi huo .